LONDON-Tanzania imeshinda tuzo kubwa za kimataifa za uhifadhi wa mazingira (Tusk for Conservation in Africa) katika hafla iliyoandaliwa usiku wa kuamkia Novemba 27, 2025 jijini London, Uingereza.
Mshindi wa tuzo hiyo ni Bi. Rahima Njaidi, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA).
Ushindi wake wa tuzo hii ya kwanza duniani umetajwa kuwa hatua muhimu inayotambua mchango wa Tanzania katika kulinda na kuhifadhi bioanuwai barani Afrika.
Tuzo za Tusk Conservation hutolewa kila mwaka kwa lengo la kuwaenzi wahifadhi wa Kiafrika walioonesha ubunifu, uongozi na athari kubwa katika kulinda mazingira.
Tangu kuanzishwa kwake miaka 13 iliyopita, tuzo hizo zinazotolewa kwa ushirikiano na Meneja wa Uwekezaji wa Ninety One na tayari zimewatambua washindi 57 kabla ya mwaka huu.
Bi. Rahima, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, ametajwa kuwa miongoni mwa viongozi wanawake mashuhuri katika sekta ya uhifadhi wa misitu.
Ana takribani miaka 20 ya kufanya kazi ya kuwawezesha wananchi wa vijijini kupitia Usimamizi wa Misitu unaotokana na Jamii (CBFM), kuimarisha utawala bora na kuchochea maendeleo endelevu.
Kupitia MJUMITA, Bi. Rahima anaongoza mtandao wenye jumla ya mashirika 132 ya kiraia (CBOs), yanayofanya kazi katika vijiji 503 nchini.
Mashirika hayo yanahusika na utetezi wa ulinzi wa misitu, uhifadhi wa bioanuwai pamoja na kuhakikisha jamii zinapata na kulinda haki zao za ardhi.
Tuzo za Tusk Conservation zimeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuibua mashujaa wa uhifadhi barani Afrika, huku zikileta hadithi zao mbele ya dunia.
Tangu mwaka 2013, tuzo hizo zimekuwa chanzo cha motisha kwa wahifadhi wengi na zimechangia kuongeza uelewa wa kimataifa kuhusu juhudi za kulinda mazingira barani Afrika.
Kwa ushindi huu, Tanzania imeimarisha nafasi yake kama taifa linalotambulika kimataifa kwa juhudi endelevu za kuhifadhi mazingira na bioanuwai.
