NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema, itaendelea kutoa mafunzo maalumu ya elimu ya uchumi na masoko ya fedha kwa waandishi wa habari nchini ili kuongeza ubora wa taarifa zinazotolewa kwa umma, kuimarisha uwazi wa kifedha na kusaidia ukuaji wa uchumi.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 19,2025 jijini Dodoma na Meneja wa Idara ya Uendeshaji, Tawi la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dodoma, Bw.Nolasco Maluli wakati akifungua semina ya siku tatu kwa waandishi wa habari za uchumi na biashara nchini.Semina hiyo ambayo inaratibiwa na BoT imewaleta pamoja waandishi wa habari kutoka mikoa mitano ikiwemo Zanzibar, Dodoma, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
Meneja wa Idara ya Uendeshaji, Tawi la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dodoma, Bw.Nolasco Maluli akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya waandishi wa habari Jijini Dodoma."Benki Kuu inatambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari nchini kupitia ninyi waandishi wa habari ambao mmekuwa na jukumu la kuandaa habari,vipindi mbalimbali na makala zinazohusiana na uchumi na fedha na umma umekuwa ukipata taarifa sahihi ambazo zimekuwa zikiwasaidia."
Pia, amesema waandishi wa habari ni daraja muhimu kati ya wataalamu wa uchumi na wananchi nchini.
Amefafanua kuwa,bila elimu sahihi, habari zinaweza kupotosha umma au kupunguza imani kwao na wawekezaji katika masoko nchini.
Bw.Maluli ameongeza kuwa, mafunzo haya ya siku tatu yatawawezesha wanahabari kufanya uchambuzi wa kina kuhusu masuala ya fedha na uchumi, hivyo kuongeza thamani ya habari wanazowalisha wananchi.
Meneja Msaidizi Uchumi wa Benki Kuu Tawi la Dodoma,Bw. Shamy Chamicha akiwasilisha mada katika semina ya waandishi wa habari inayofanyika jijini Dodoma
Meneja Msaidizi wa Uhusiano wa Umma Benki Kuu ya Tanzania, Bi.Noves Moses akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya waandishi wa habari inayofanyika jijini Dodoma.Ikumbukwe kuwa,Benki Kuu ya Tanzania ina mchango mkubwa katika maendeleo ya masoko ya fedha nchini kwa kujenga mazingira wezeshi.
Vilevile,mchango wa Benki Kuu umejikita hasa katika kutoa miundombinu ya masoko ya fedha, kuhakikisha kuna sheria zinazotakiwa, kusimamia na kujenga nyenzo za masoko.
Washiriki katika semina hii, watapata fursa ya kujifunza kuhusu mada mbalimbali ikiwemo muundo na majukumu ya Benki Kuu, maana ya Sera ya Fedha inayotumia Riba ya Benki Kuu,elimu ya hatifungani na umuhimu wake katika Taifa.
Mada nyingine ni elimu kuhusu huduma ndogo za fedha na usajili wa vikundi, namna ya kumlinda mtumiaji wa huduma za fedha (SEMA NA BOT), namna BoT inavyosimamia mifumo ya malipo nchini na utambuzi wa alama za usalama katika noti.

