DAR-Wataalamu kutoka Benki Kuu ya Rwanda (BNR) wametembelea Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kujifunza namna BoT inavyotengeneza na kuendesha mifumo ya TEHAMA kwa kutumia wataalamu wa ndani, pamoja na kubadilishana uzoefu katika masuala ya teknolojia.

Ziara hiyo, iliyofanyika kuanzia tarehe 24 hadi 27 Novemba 2025 katika makao makuu ya BoT jijini Dar es Salaam, ililenga kuwapa uelewa wa mbinu bora zilizosaidia BoT kufanikisha matumizi ya mifumo ya kidijitali, sambamba na mikakati ya kuongeza ufanisi katika usimamizi wa nyaraka ndani ya taasisi za kifedha.
Katika ziara hiyo, wataalamu kutoka Rwanda walijengewa uelewa kuhusu utengenezaji na uendeshaji wa mifumo ya TEHAMA ndani ya BoT, taratibu za uthibitishaji wa ubora, pamoja na hatua mbalimbali zinazotekelezwa ili kuhakikisha usalama na uthabiti wa mifumo hiyo.
Aidha, walipata fursa ya kutembelea Makumbusho ya Benki Kuu ya Tanzania, ambapo walijifunza kuhusu historia ya fedha nchini pamoja na safari ya BoT tangu kuanzishwa kwake tarehe 14 Juni 1966.


