ARUSHA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeratibu mkutano wa Kamati ya Ufundi ya Tehama katika Masuala ya Fedha (MAC -IT Technical Workgroup) kwa Benki Kuu za nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mkutano huo wa siku nne umefunguliwa leo Jumatatu Novemba 24, 2025 na Meneja wa Idara ya Uchumi, Tawi la BoT Arusha, Bw. Aristides Mrema kwa niaba ya Mkurugenzi wa tawi hilo.
Mrema amesema, katika kipindi cha hivi karibuni teknolojia imepiga hatua ikiwemo matumizi makubwa ya Akili Unde (AI), hivyo haina budi kwa Benki Kuu nazo kujua namna ya kujikinga na hatari mpya za kimtandao zinazoendana na maendeleo hayo ya teknolojia.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Mifumo ya Mawasiliano BoT, Bw. Joel Ngussa amesema lengo kuu la warsha hiyo ni kubadilishana uzoefu, ulinganifu wa usimamizi wa TEHAMA, na kuandaa mapendekezo yanayoweza kutekelezeka ambayo yataimarisha usimamizi wa mifumo katika Benki Kuu wanachama.Mkutano huo umehudhuriwa na wajumbe kutoka nchi wananchama za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni; Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Somalia, Sudani Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.



