DAR-Kampuni ya mabasi ya Esther Luxury Coach Limited imetangaza kurejesha rasmi huduma zake za usafirishaji wa abiria kuanzia leo Novemba 6, 2025, baada ya kusitisha safari kwa muda kufuatia changamoto zilizotokana na vurugu za maandamano ya hivi karibuni.
Kupitia taarifa yake kwa umma, kampuni hiyo imesema ililazimika kusimamisha huduma kwa muda mfupi ili kuratibu athari zilizojitokeza, na sasa imerejea kwa nguvu mpya na huduma bora zaidi.
"Baada ya kupitia kipindi kigumu kilichosababisha baadhi ya mali zetu kuathiriwa, tunawajulisha wateja wetu na Watanzania kwa ujumla kuwa huduma zetu zimerejea kama kawaida kuanzia Novemba 6, 2025,”imesema taarifa hiyo.
Kampuni hiyo ambayo inamilikiwa na wazawa Joseph Didas Ngeleuya na Neema Peter Thomas, kama inavyoainishwa kwenye nyaraka za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imesema inaendelea kujivunia uwekezaji wake katika sekta ya usafirishaji nchini.
"Misingi yetu imejengwa katika usalama, ubora, ubunifu na heshima kwa kila mteja. Esther Luxury Coach-The Real Choice."

