DAR-Askofu wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Mashariki, Lawi Mwankuga amewataka Watanzania kuacha kulaumiana na badala yake kujikita katika kuthamini Utaifa wetu.
Askofu Lawi Mwankuga ameyasema hayo leo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kwaya ya Jimbo hilo unaofanyika katika Ushirika wa Tabata jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo ulipangwa kudanyika tarehe 31 Oktoba hadi 2 Novemba, lakini haukufanyika kutokana na maandamano na vurugu zilizotokea kuanzia siku ya Uchaguzi Mkuu tarehe 29 Oktoba na kusababisha upotevu wa maisha, majeruhi pamoja na mali katika maeneo mengi nchini.
"Majira yaliyopelekea mabadiliko ya kufanya mkutano huu, yalipelekea vilio vingi, maumivu mengi na mashaka mengi katika eneo ambalo tunaishi. Mungu aendelee kutuhurumia," ameeleza Askofu Mwankuga.
"Mungu wa faraja aendelee kuwa faraja kwa wote. Wengine wamepata umauti, wengine wamepata ulemavu, na wengine hatujui wako wapi. Mungu aendelee kuwa haki kwa Watanzania, amesema kiongozi huyo wa dini."
Aidha, amesoma Zaburi 46 na kuhimiza kwamba kimbilio letu la kweli ni Mungu, kwani yeye anaweza yote.
Askofu Mwankuga amesema wakati mwingine wanadamu wanakimbilia wanadamu wenzao, au serikali, au bunge au watu wengine, lakini hao wanaowakimbilia nao wanapaswa kumkimbilia Mungu.
"Tumuombe Mungu atuhurumie, atusaidie, tuendelee kuishi katika hali ambayo ni hali ya kuishi,"amesema Askofu Mwankuga.
Katika Mkutano huo kuna jumla ya kwaya tatu zenye zaidi ya waimbaji 150, mbili kutoka Dar es Salaam na moja kutoka Morogoro. Ambapo wanaimba na kubadilishana vipawa vya uimbaji.Kwaya hiyo ya jimbo iko chini ya uongozi wa Mwalimu Gwantwa Kyangwe.

