LUANDA-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi atamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Saba wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Ulaya (EU) unaotarajiwa kufanyika jijini Luanda, Angola kuanzia tarehe 24 na 25 Novemba 2025.
Mkutano huo ambao umeanza jijini hapa Novemba 23, 2025 kwa Ngazi ya Maafisa Waandamizi kutoka AU na EU, pamoja na mambo mengine utajadili utekelezaji wa Dira ya Pamoja ya 2030 kama ilivyopitishwa kwenye Mkutano wa Sita wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa AU-EU uliofanyika mwaka 2022.
Vilevile namna ya kuimarisha ushirikiano kupitia miradi ya kiuchumi na kimkakati hususan, katika sekta za nishati, miundombinu na shoroba za usafirishaji, mifumo ya kidijitali, uboreshaji wa sekta ya kilimo.
Pia elimu,afya na uendelezaji wa rasilimali watu inayotekelezwa chini ya ajenda ya Global Getaway Partneship.
Kadhalika Mkutano huo utajadili ripoti ya utekelezaji wa Azimio la Mkutano wa Sita uliofanyika Brussels, Ubelgiji, mwaka 2022 na pia kufanya majadiliano kwenye mada mbalimbali ikiwemo Ustawi na Maendeleo endelevu kwa Afrika na Ulaya; Kuimarisha ushrikinao kwenye masuala ya amani, usalama na Utawala bora; Kuimarisha Ushirikiano kwenye masuala ya uhamaji na uhamiaji pamoja na Kuongeza utashi kwenye masuala ya Kimataifa.
Wakizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Maafisa Waandamizi, Wenyeviti Wenza wa Mkutano huo Mhe. Balozi Miguel Cesar Domingos Bembe kutoka AU na Mhe. Balozi Patricia Lombart Cussac kutoka EU wamewataka wajumbe wa mkutano huo kujadili na kupitia agenda zilizowasilishwa kwao kwa kabla ya kuwasilishwa kwa Wakuu wa Nchi kwa ajili ya kuridhiwa kwa maslahi mapana ya Jumuiya hizi mbili.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Maafisa Waandamizi umeongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu kwenye Umoja wa Afrika, Mhe. Innocent Shiyo.










