DAR-Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na wadau imeanza mchakato wa uorodheshaji wa matumizi ya vazi la kanga kwenye orodha ya kitaifa ya urithi wa utamaduni usioshikika, ili kuteuliwa kuingizwa kwenye orodha ya Urithi wa Dunia unaosimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Mchakato huo umeanza kwa kuratibiwa kwa warsha ya wadau wa utamaduni kutoka Tanzania Bara na Zanzibar iliyofanyika tarehe 11 Novemba, 2025 jijini Dar es Salaam.Katika warsha hiyo, wadau walipata fursa ya kujadili chimbuko la Kanga na matumizi yake katika miktadha mbalimbali ya kiutamaduni wa Mtanzania na shughuli za kila siku.
Akifungua warsha hiyo, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Utamaduni wa Wizara hiyo, Dkt. Julieth Kabyemela amebainisha kuwa, kuorodheshwa kwa vazi la Kanga kama sehemu ya urithi wa utamaduni usioshikika, kutasaidia kuimarisha ushirikiano baina ya Mataifa katika kulinda urithi wa utamaduni usioshikika pamoja na kutangaza utalii wa kiutamaduni kimataifa.
Warsha hiyo imewakutanisha washiriki mbalimbali wakiwamo; wataalamu kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Wizara Ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo-Zanzibar, Ofisi ya UNESCO Dar es Salaam, wahadhiri kutoka vyuo vikuu nchini, asasi za kiraia, sekta binafsi, wawakilishi wa jamii mashirikisho ya kazi za sanaa na Taasisi zilizoko chini ya Wizara.













