Miradi ya NHC yafungua fursa mpya kiuchumi,makazi bora na kijamii Dar

NA MWANDISHI WETU

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) linaendelea kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya makazi nchini kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati inayolenga kuongeza upatikanaji wa nyumba bora, za kisasa na zenye viwango vya kimataifa.
Mradi wa Kawe 711 ni kielelezo cha ubunifu na ustawi wa maisha ya kisasa jijini Dar es Salaam. Ukiwa ni mojawapo ya miradi mikubwa ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Kawe 711 umebuniwa kwa ustadi ili kutoa mchanganyiko kamili wa makazi bora, burudani na uwekezaji wenye tija. 📞 Wasiliana nasi kwa maelezo zaidi: +255 736 114 433 au 🌐 Tembelea: www.nhc.co.tz

Miradi hiyo, inayotekelezwa jijini Dar es Salaam na maeneo mengine nchini, inahusisha ujenzi wa makazi, maeneo ya biashara na ofisi kwa ubora unaokidhi mahitaji ya sasa ya mijini.

Kupitia mpango wake wa muda mrefu, NHC inaendeleza miradi ya ndani ya shirika, miradi ya ubia, pamoja na miradi inayopewa kupitia zabuni na Serikali pamoja na taasisi nyingine za umma.

Miongoni mwa miradi iliyopewa kipaumbele ni Samia Housing Scheme Kijichi, Mradi wa Ubia wa NHC Kariakoo, na Mradi wa Kawe 711, yote ikiwa jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa za NHC, utekelezaji wa miradi hiyo unafanyika sambamba na dira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora, salama na endelevu.

Shirika limeweka mkazo katika matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira, zenye gharama nafuu na zinazoongeza ustahimilivu wa majengo.

SAMIA HOUSING SCHEME KIJICHI

Moja ya miradi mikubwa na ya kimkakati inayotekelezwa kwa kasi na NHC ni Samia Housing Scheme Kijichi katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Mhandisi wa Mradi, Julieth Prosper anabainisha kuwa,mradi huo unajumuisha ujenzi wa majengo 12 yenye jumla ya nyumba 260.
Nyumba hizo zimegawanyika katika majengo matano ya nyumba za vyumba vitatu, majengo ya matano ya nyumba za vyumba viwili na majengo mawili ya nyumba za chumba kimoja.

Nyumba zote zitakuwa na sebule, jiko na miundombinu ya kisasa ili kukidhi mahitaji ya familia za aina mbalimbali.

Kwa upande wa usimamizi wa ujenzi, Mhandisi Elias John anafafanua kuwa,mradi huo utakuwa na zaidi ya maeneo 300 ya maegesho yakihakikisha kila nyumba inapewa nafasi yake pamoja na jengo maalum litakalojumuisha maduka, huduma za kijamii na benki kupitia mashine za ATM. Hii inalifanya eneo hilo kuwa kitovu kamili cha makazi.

Mradi ulianza kutekelezwa Agosti 22, 2025 na unatarajiwa kukamilika Agosti 22, 2027, kwa gharama ya shilingi bilioni 41.5.

Mwitikio Chanya

Kwa upande wa mauzo, Ofisa Mauzo na Masoko Mkuu wa NHC, Daniel Kure anasema,mwitikio wa wananchi ni wa kuridhisha, ambapo tayari kati ya asilimia 15 hadi 20 ya nyumba zimekwishauzwa licha ya mradi kuanza hivi karibuni.
Kure anaeleza kuwa,NHC imeweka utaratibu rahisi unaowawezesha wananchi kumiliki nyumba kupitia njia tatu za malipo ikiwemo malipo ya fedha taslimu kuanzia asilimia 10 ya thamani ya nyumba.

Pia,malipo kwa awamu ndani ya miezi sita hadi miaka miwili na mikopo ya nyumba (mortgage) kupitia zaidi ya taasisi 20 za kifedha zinazoshirikiana na NHC.

Kwa mfano, nyumba yenye thamani ya Shilingi milioni 220 inaweza kumilikiwa kwa kuanza na Shilingi milioni 22, huku taasisi za fedha zikigharamia kiasi kilichobaki kwa masharti nafuu.

Bei za nyumba katika mradi ni chumba kimoja shilingi milioni 112,vyumba viwili shilingi milioni 220 na vyumba vitatu shilingi milioni 335.

Kure anawataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo, akisisitiza kuwa eneo la Kijichi liko karibu kuliko inavyodhaniwa, likifikika kwa njia mbili kuu kupitia Daraja la Kigambon,Kibada hadi Kijichi.

Aidha,kupitia Barabara ya Kilwa,Mbagala Misheni ikiwa ni umbali wa kilomita 15 tu kutoka katikati ya jiji.

Kwa mujibu wa NHC, kukamilika kwa mradi wa Samia Housing Scheme Kijichi kutachochea ukuaji wa thamani ya ardhi katika eneo hilo, pamoja na kufungua milango ya fursa mpya za biashara, ajira na maendeleo ya kijamii ikiwa ni sehemu ya juhudi endelevu za kuboresha makazi nchini.

MRADI WA UBIA WA NHC KARIAKOO

Mradi wa Ubia wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) unaotekelezwa katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam umeendelea kuwa mfano halisi wa namna ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi unavyoweza kuharakisha maendeleo ya mijini.
Elizabeth Maro ambaye ni Meneja wa Miradi ya Ubia wa NHC anaeleza kwamba,kuanzia mwaka 2024 NHC imeingia makubaliano ya kutekeleza miradi 21 ya ubia katika eneo la Kariakoo.

Kati ya hiyo, amesema miradi mitano ipo hatua za mwisho na mingine mitano imeshapata kibali cha matumizi kamili.

Aidha,kupitia mikataba hiyo ya ubia, maeneo ya zamani ya biashara yameanza kubadilishwa kuwa majengo ya kisasa yenye matumizi mchanganyiko, hatua inayoongeza mvuto wa wafanyabiashara na kuchochea shughuli za kiuchumi katika jiji la Dar es Salaam.
Jambo la kuvutia ni kwamba miradi hii imeanza kuzalisha mapato ndani ya mwaka mmoja, kinyume na matarajio ya awali yaliyokadiria uingizaji wa mapato baada ya miaka miwili.

Kwa sasa NHC ina miradi 23 inayotekelezwa na zaidi ya maombi 100 ya ubia kutoka kwa wawekezaji.

Makadirio mapya yanaonesha kuwa,miradi hiyo, ikiwa imekamilika kwa asilimia 25 tu, itaingiza zaidi ya shilingi bilioni 6 kwa mwaka, mara tatu ya makadirio ya awali ya Sh bilioni 2.

Hii inamaanisha kuongezeka kwa mapato ya NHC pamoja na mapato ya Serikali kupitia kodi na gawio, hivyo kuchochea uchumi wa taifa.

Sifa kuu za mradi

Moja ya alama kubwa za mradi huu ni mfumo wa matumizi mchanganyiko, ambapo majengo yanabeba makazi, biashara, ofisi na huduma mbalimbali katika eneo moja. Hii inaunda mazingira ya biashara yenye ufanisi na urahisi kwa wananchi.

Sifa ya pili ni ujenzi unaolenga kuongeza thamani ya Kariakoo kama kitovu cha biashara, hatua itakayochochea uchumi wa eneo hilo na kulifanya liendelee kuwa kitovu cha shughuli za biashara jijini Dar es Salaam.

Sifa ya tatu ni ubunifu wa usanifu, ambao unajumuisha majengo yenye nafasi pana, viwango vya juu vya usalama, taa za kisasa, na mifumo bora ya usimamizi wa taka.

Aidha,uboreshaji huu unalenga kutoa mazingira salama na ya kisasa kwa wakazi na wafanyabiashara.
Pia, mradi umejikita katika dhana ya uwekezaji unaozalisha mapato mapema, ambapo taarifa kutoka Kitengo cha Miradi ya Ubia cha NHC zinaonesha kuwa baadhi ya miradi imeanza kuingiza mapato kabla ya muda uliopangwa. Hii inaonesha uimara wa usimamizi na ufanisi wa utekelezaji wa miradi hiyo.

Sifa ya tano inayolifanya eneo hili kuwa la kipekee ni kwamba mradi umefungua fursa kwa wawekezaji zaidi ya 100 walioonyesha nia ya kushirikiana na NHC katika shughuli za kibiashara.

Mwitikio huu mkubwa unaashiria kuongezeka kwa imani ya sekta binafsi kwa Shirika la Nyumba la Taifa.

Kwa ujumla, Mradi wa Ubia Kariakoo unatajwa kuwa nguzo muhimu katika mageuzi ya maeneo ya biashara Dar es Salaam, huku ukitarajiwa kuongeza mapato ya NHC na serikali kupitia kodi, gawio na ongezeko la shughuli za kiuchumi.

Mradi huu unaashiria mwelekeo mpya wa ukuzaji wa miji unaotokana na ushirikiano wa kimkakati kati ya sekta binafsi na serikali.


Mradi wa Kawe 711 ambao unatekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) umeendelea kuwa miongoni mwa alama mpya zinazoifanya Dar es Salaam kung’ara kama jiji la kisasa na linalokua kwa kasi.
Ujenzi wa majengo mawili ya ghorofa 17 umepiga hatua kubwa, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya kazi tayari imekamilika, ikiwa ni ishara na mwelekeo wa Watanzania kuendelea kuishi katika maeneo salama, yenye mandhari ya kuvutia na huduma za kisasa.

Sifa za kipekee zinazoubeba mradi

Mradi wa Kawe 711 unaangazia ubunifu na ubora kupitia sifa tano mahsusi ambazo zinauweka katika daraja la miradi ya makazi ya kiwango cha juu zaidi nchini.

1. Miundombinu ya kisasa na usanifu wa Kimataifa

Majengo yake marefu ya ghorofa 17 yanajengwa kwa teknolojia ya kisasa, yakionesha mwelekeo mpya wa maendeleo ya mijini na kuleta sura ya kimataifa katika eneo la Kawe.

2. Makazi ya hadhi ya juu

Mradi unatoa chaguzi mbalimbali za makazi, ikiwemo vyumba 2, 3 na 4 vilivyopangwa kwa ubunifu mkubwa ili kutoa nafasi za kuishi zisizochosha na zinazokidhi mahitaji ya familia za kisasa.

3. Eneo lenye huduma za burudani na afya

Kawe 711 umejengwa kwa kuzingatia ustawi wa wakazi wake kupitia uwepo wa mabwawa ya kuogelea, kumbi za mazoezi, maeneo ya watoto na bustani zinazoongeza utulivu na mvuto wa makazi.

4. Huduma za kibiashara ndani ya mradi

Uwepo wa maduka, huduma za kibenki na maeneo ya ofisi ndani ya mradi unarahisisha maisha ya wakazi kwa kuwapatia huduma muhimu bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

5. Maegesho ya kutosha

Mradi umewekeza katika miundombinu ya maegesho ya kutosha kwa wakazi, wageni na magari ya ziada ya familia, hatua inayoongeza usalama na urahisi wa matumizi ya nafasi za makazi.

Kwa ujumla, Kawe 711 ni mradi uliobuniwa na NHC kwa kuzingatia mahitaji ya familia za kipato cha kati zinazotafuta ubora wa maisha katika mazingira yenye mandhari ya kuvutia.

Mbali na kuboresha viwango vya maisha, mradi huu unachochea ongezeko la thamani ya ardhi na kusukuma mbele shughuli za kiuchumi Kawe na maeneo jirani, hivyo kuifanya kuwa mojawapo ya sehemu bora zaidi kuwekeza katika makazi jijini Dar es Salaam.

Ofisa Mauzo na Masoko Mkuu wa NHC, Daniel Kure. anaeleza kuwa,mradi huu mkubwa unahusisha ujenzi wa nyumba 400 na unatarajiwa kukamilika Aprili 2026.

Amesema,majengo yana ghorofa 17 na yapo mita 300 tu kutoka baharini. Mauzo yameanza tangu mwaka jana na mwitikio ni mkubwa kutokana na ubora wa majengo na hatua za mwisho za ujenzi zinazoendelea.
Wananchi wanahimizwa kutembelea eneo la mradi ambako maofisa mauzo wapo tayari kutoa huduma za papo kwa hapo.

FAIDA ZA KIJAMII NA KIUCHUMI ZA MIRADI YA NHC

Miradi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) imeendelea kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini, ikiwa na mchango mpana unaogusa maisha ya wananchi kwa namna mbalimbali.

Mosi, miradi hii imekuwa ikitoa fursa nyingi za ajira kwa vijana katika sekta za ujenzi, usimamizi wa miradi,usafirishaji na huduma nyingine zinazohusiana na shughuli za miji.

Aidha,kupitia ajira hizi, uchumi wa kaya umeimarika na kuongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za uzalishaji.

Pia,utekelezaji wa miradi ya NHC umechochea kwa kiasi kikubwa ukuaji wa biashara ndogondogo na za kati katika maeneo jirani, ikiwemo huduma za chakula, uuzaji wa vifaa vya ujenzi, usafirishaji na huduma nyingine za kiamii. Hali hii imekuwa na msukumo chanya kwa maendeleo ya sekta binafsi.
Miradi hii pia imechangia kuongeza thamani ya ardhi katika maeneo yanayozunguka ujenzi, hivyo kuibua fursa mpya za uwekezaji na kuleta mpangilio bora wa matumizi ya ardhi katika miji mbalimbali nchini.

Kupitia nyumba za kisasa na salama zinazojengwa, NHC imetoa fursa kwa wananchi kupata makazi bora yenye hadhi, yanayokidhi mahitaji ya maisha ya sasa.

Vilevile, shirika limekuwa mstari wa mbele kuwawezesha wapangaji kugeuka wamiliki wa makazi kupitia mipango shirikishi ya ununuzi wa nyumba.

Kwa ujumla, mchango wa NHC kupitia miradi yake unaendelea kuboresha maisha ya wananchi na kuleta sura mpya ya maendeleo katika miji ya Tanzania, huku ikiimarisha ustawi wa kijamii na kukuza uchumi wa taifa.

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linaendelea kuwa kielelezo cha maendeleo katika sekta ya makazi nchini.

Kuanzishwa kwake miaka zaidi ya 60 iliyopita kulikuwa na lengo la kushughulikia upatikanaji wa nyumba kwa wananchi na kukuza makazi ya kisasa.

Tangu wakati huo hadi leo, NHC limekuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa miradi ya makazi, biashara na ofisi, sambamba na kushirikiana na serikali, taasisi za umma na wadau mbalimbali nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news