NA DIRAMAKINI
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemchagua, Mhe. Mussa Azzan Zungu kuwania nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kushinda kwa kishindo katika uchaguzi wa ndani ya chama uliofanyika jijini Dodoma.
Katika uchaguzi huo wa ndani ya chama, jumla ya kura 364 zimepigwa,na hakukuwa na kura hata moja iliyoharibika, jambo lililoashiria nidhamu na uwazi mkubwa katika mchakato huo wa kidemokrasia.
Matokeo rasmi yametangazwa kwamba Mhe. Zungu amepata kura 348, akimshinda mpinzani wake Mhe. Stephen Masele, ambaye amepata kura 16 pekee.
Ushindi huo mkubwa unamuweka Mhe. Zungu katika nafasi ya kushinda kuwa Spika wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akichukua nafasi ya mtangulizi wake, Mheshimiwa Dkt.Tulia Ackson ambaye alijiondoa katika kinyang’anyiro hicho.
Aidha,wadau mbalimbali wamempongeza Mheshimiwa Zungu wakisema ushindi huo ni ishara ya umoja ndani ya chama na chombo hicho cha kutunga sheria na matumaini ya kuimarisha zaidi misingi ya demokrasia nchini.
Pia, kitaaluma, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema matokeo hayo yanaonesha kuimarika kwa taasisi za kidemokrasia na uwazi wa mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Bunge.
Mheshimiwa Zungu ambaye pia ni Mbunge wa Ilala (CCM) jijini Dar es Salaam amewahi kushika nyadhifa kadhaa serikalini ikiwemo kuwa Naibu Waziri,Naibu Spika na Mwenyekiti wa Kamati mbalimbali za Bunge, hivyo uzoefu wake unatarajiwa kuleta ufanisi katika uongozi wa shughuli za Bunge.
Kwa upande wa nafasi ya Naibu Spika, Mbunge Daniel Silo ameibuka kinara baada ya kupata kura 362, huku wagombea wengine waliokuwa wamejitokeza awali wakijiondoa kabla ya zoezi la upigaji kura kuanza.
