ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi wenye mitaji mikubwa kuja kuwekeza nchini.
Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Novemba 19, 2025, wakati akifungua rasmi Hoteli ya TEMBO KIWENGWA ZANZIBAR RESORT iliyopo Kiwengwa, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amesema sekta ya utalii inaendelea kukua kwa kasi, na Zanzibar tayari imevunja rekodi ya idadi ya wageni. Kufikia mwezi Oktoba 2025, takribani wageni 743,000 wamewasili nchini.
Amesema,hali ya utulivu na amani kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu imechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa idadi hiyo, na Serikali inaendelea na azma yake ya kufikia wageni milioni moja kwa mwaka.
Kuhusu uwekezaji wa hoteli hiyo, Rais Dkt Mwinyi ameeleza kufurahishwa na hatua ya wawekezaji wazawa kuwekeza kwenye miradi mikubwa yenye manufaa kwa Taifa, na kuwataka wawekezaji wengine kuiga mfano huo badala ya kubaki watazamaji katika sekta ya utalii.
Ameongeza kuwa, wawekezaji kama hao wanasaidia kutimiza dhamira ya Serikali ya kuzalisha ajira 350,000 kwa vijana, kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya CCM.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameipongeza Menejimenti ya hoteli hiyo kwa kuwaunga mkono wajasiriamali wa eneo la Kiwengwa kwa kuwapa masoko ya uhakika ya bidhaa mbalimbali ikiwemo samaki, mbogamboga, na bidhaa nyingine zinazotengenezwa na wajasiriamali wadogo.
Amesisitiza kuwa, Serikali itaendelea kutoa msamaha wa kodi kwa wawekezaji ili kuwahamasisha zaidi kuwekeza katika sekta mbalimbali za kiuchumi.
Mradi wa TEMBO KIWENGWA ZANZIBAR RESORT umegharimu jumla ya Dola za Marekani milioni 12, una vyumba 95 vya hadhi ya juu, uwezo wa kuhudumia wageni 200 kwa wakati mmoja, na umechangia ajira 145 kwa wazawa.





















