NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kuendelea kudhibiti vitendo vya rushwa nchini ili rasilimali za nchi ziweze kuwanufaisha zaidi wananchi.


"Tumezungumzia masuala mengi, ila msingi wa mafanikio yote haya ni utawala wa sheria, uadilifu na uwajibikaji katika kila ngazi, kuanzia juu mpaka chini.
"Kwa msingi huo, na ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali za nchi pamoja na kupata huduma wanazostahili, tutaelekeza jitihada zetu kwenye mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi, ubadhirifu, uzembe, ukosefu wa nidhamu na ukosefu maadili.
"Ni lazima tudhibiti wachache wanaotaka kuturudisha nyuma kwa kuendekeza maslahi binafsi."
Aidha, Rais Dkt.Samia amesema, ili kuimarisha uwajibikaji serikalini, wataendelea kutekeleza programu za maboresho ya utumishi wa umma, ikiwemo matumizi ya mifumo ya upimaji wa utendaji kazi.
"Wajibu huenda na haki, au haki huambatana na wajibu.Hivyo basi, pamoja na kuwataka watumishi wa umma kuwajibika ipasavyo, tutaendelea kuboresha maslahi yao kadri uchumi utakavyoruhusu."
Pia amesema, Serikali itaimarisha uwajibikaji na utendaji wa mashirika ya umma.
"Kuelekea 2030, tutafanya mageuzi ya mashirika ya umma ili kuboresha ufanisi, uwazi na tija. Tunataka kuongeza sio tu gawio ambalo Serikali inapokea, lakini pia kufikia lengo la Mashirika na Taasisi za Umma kuchangia angalau asilimia 10 ya mapato yote yasiyo ya kodi.
"Nia yetu ni kuyajengea uwezo Mashirika ya Umma yaweze kushindana na kuwekeza nje ya Tanzania, kama mashirika mengine ya nje tunavyoyaona hapa nchini kwetu."
Katika hatua nyingine, Rais Dkt.Samia amesema kuwa, msingi mwingine wa mafanikio yote haya ni utawala wa sheria.
"Ahadi yetu ni kuwa Serikali itashirikiana kwa dhati na Mahakama ya Tanzania kuhakikisha haki inapatikana kwa watu wote na kwa wakati.
"Tutaendelea kuwezesha Mahakama kwa majengo, vitendea kazi, watumishi pamoja na kuimarisha matumizi ya TEHAMA. Tunachukua hatua zote hizi ili Mhimili huu uweze kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi.
"Tutasimamia utekelezaji kamili wa mapendekezo ya Tume ya Rais ya kuangalia namna ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai. Tutaendelea kufanya mageuzi na maboresho katika taasisi zote zinazoshughulikia masuala ya Haki Jinai ili ziweze kukabiliana na vitendo vyote vya uhalifu."
Kwa upande mwingine, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta ya Sheria ikiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Sambamba na asasi zingine ili kuwezesha upatikanaji wa huduma na msaada wa kisheria kwa wananchi, kwani katika kipindi kilichopita wameona manufaa yake katika utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Aidha, amesema watakamilisha tafsiri ya sheria zote kwa lugha ya Kiswahili, ikiwa ni hatua muhimu kuhakikisha wananchi wanaelewa kwa urahisi sheria za nchi.
Tags
Bunge la Tanzania
Dr Samia Suluhu Hassan
Habari
PCCB Tanzania
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
