Serikali kuanzisha wizara kamili ya vijana Tanzania

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuanzisha wizara kamili itakayoshughulikia masuala ya vijana.
Amesema hayo leo, tarehe 14 Novemba 2025, wakati akilihutubia Bunge la 13 jijini Dodoma na kuelezea mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita katika mhula wa pili.

Dkt. Samia amesema pia atahakikisha kunakuwepo na Washauri Maalum wa Rais kuhusu masuala ya vijana.

“Katika kuhakikisha tunaondoa changamoto za vijana, dhamira yangu ni kuhakikisha tunaanzisha Wizara rasmi inayoshughulikia masuala ya vijana,” amesema.

Amesema pia dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Bima ya Afya kwa Wote inamnufaisha kila Mtanzania. “Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha tunatekeleza Bima ya Afya kwa Wote na kuhakikisha kila Mtanzania anapata matibabu bila changamoto yoyote,” amesema.

Dkt. Samia ametoa wito kwa Watanzania kuchangamkia Bima ya Afya kwa Wote ili kupata matibabu bila vikwazo, hata kama hawana fedha pindi wanapoumwa.

Aidha, Serikali itajenga Hospitali Maalum ya Magonjwa ya Mlipuko mkoani Kagera. Kuhusu uimarishaji wa miundombinu ya afya, Dkt. Samia amesema ujenzi na uboreshaji wa vituo vya kutolea huduma utaendelea ili kila mwananchi apate huduma karibu na eneo analoishi.

“Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha huduma za afya zinakuwa karibu zaidi na wananchi, hivyo tutahakikisha ujenzi wa Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati unaendelea ili kuleta ufanisi wa huduma,” amesema.
Aidha, Rais Samia amebainisha kuwa Serikali ina dhamira ya kuhakikisha hakuna mtu yeyote atakayezuia maiti hospitalini. “Tunaweka utaratibu maalum mtu aruhusiwe kumzika mpendwa wake na si kuzuia maiti, hivyo bora achukue alipe kidogo kidogo,” amesema Dkt. Samia.

Wakati huo huo, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amezungumzia hali ya kisiasa nchini Tanzania baada ya uchaguzi, akisisitiza umuhimu wa amani, umoja, na demokrasia katika maendeleo ya taifa.

Pia ametoa wito kwa Watanzania wote, hususan vijana kuzingatia maelewano na ushirikiano katika kipindi hiki cha changamoto.

Amekumbusha kuwa nchi ya Tanzania imejengwa kwenye misingi ya amani na utulivu wa kisiasa, na kwamba kama vijana watashindwa kujali na kulinda misingi hii, taifa litaathirika zaidi.

Amewaambia vijana kuwa, nchi yao ni yao wenyewe, na kwamba hawapaswi kuharibu kile kilichojengwa kwa jasho na damu za wazee wao.

Rais Samia ameongeza kuwa, vijana ni nguzo ya taifa, na hivyo wanapaswa kuwa walinzi na wajenzi wa maendeleo.
Vilevile ametoa angalizo kuwa wakati mwingine vijana wanaweza kushawishika kufanya vitendo vya uhalifu kutokana na ushabiki au kushindwa kutambua madhara ya vitendo hivyo.

Amewahimiza vijana kutoshawishika na mikumbo ya uhalifu au vurugu, akisema kuwa umoja na amani ni muhimu kuliko chochote.

Kwa upande mwingine, Rais Samia ameeleza kwamba,anafahamu kuwa vijana wengi waliokamatwa kwa makosa ya uhaini hawakujua madhara ya vitendo vyao.

Kama Mama na Mlezi wa Taifa, ameelekeza vyombo vya sheria, hasa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, kufanya tathmini ya makosa yaliyofanywa na vijana hao, na kwa wale waliokuwa wakifuata mkumbo, ametoa ombi la kuachiliwa huru.

Kwa kuzingatia maneno ya Biblia katika Kitabu cha Luka, sura ya 23, mstari wa 34, ambapo Yesu alisema, "Baba uwasamehe kwa kuwa hawajui watendalo," Rais Samia amesisitiza msamaha kama njia ya kujenga amani na kuelewa makosa yaliyotendeka.

Pia amekumbusha kuwa,Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia, lakini demokrasia yenyewe ni mchakato unaoendelea, na inahitaji kujirekebisha kila wakati.

Amesisitiza kuwa, ili taifa liendelee kuwa na utulivu na maendeleo, ni muhimu kujifunza kutokana na mapito ya zamani na kuzingatia tamaduni, mila, na desturi zetu katika uendeshaji wa nchi.
Rais amewahakikishia wananchi kuwa serikali yake itaendelea kusimamia na kuimarisha demokrasia kwa kuzingatia misingi ya umoja, haki, na usawa.

Kama sehemu ya juhudi za kuleta umoja, Rais Samia ameongezea kuwa,serikali itatekeleza ahadi ya kufanya marekebisho ya Katiba ya Tanzania, kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2025 hadi 2030.

Amesema kuwa,mchakato wa marekebisho ya Katiba utaanzishwa kwa kuunda Tume ya Usuluhishi na Maelewano, na kwamba hili litakuwa ni hatua muhimu katika kufanikisha lengo la kukuza maelewano, umoja, na demokrasia kamili nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here