Sita wajitosa kuvaa viatu vya Spika Dkt.Tulia Ackson bungeni

DODOMA-Zoezi la Uteuzi wa Wagombea wa Uchaguzi wa Spika limekamilika leo tarehe 10 Novemba, 2025 saa 10:00 Alasiri ambapo wagombea sita kutoka vyama vya Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Chama cha National League for Democracy (NLD), Chama cha Democratic Party (DP), Chama cha Alliance for Africa Farms Party (AAFP) na Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) wameteuliwa kuwania nafasi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya leo Novemba 10, 2025 iliyotolewa na Katibu wa Bunge na Msimamizi wa Uchaguzi, Baraka Leonard imetaja majina ya wagombea hao ambao ni Mhe. Mussa Azzan Zungu (CCM), Veronica Charles Tyeah (NRA), Anitha Alfan Mgaya (NLD), Chrisant Nyakitita (DP), Ndonge Said Ndonge (AAFP) na Amin Alfred Yango (ADC).

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, kesho Novemba 11, 2025 baada ya shughuli za Bunge majina ya Wagombea walioteuliwa yatawasilishwa kwa Wapiga kura ambao ni Wabunge Wateule wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili Uchaguzi ufanyike kwa mujibu wa utaratibu utakaotolewa wakati wa Uchaguzi

Uchaguzi wa Spika unafanywa kwa mujibu wa Ibara ya 86 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Kanuni ya 9 na Nyongeza ya Kwanza ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2025 ambapo vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu vinavyokusudia kusimamisha mgombea katika uchaguzi huo vilijulishwa kuhusu kuwasilisha jina la mgombea husika ofisini kwa Katibu wa Bunge jijini Dodoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news