TAHA yatajwa kuchochea mafanikio ya sekta ya horticulture nchini Tanzania

NA GODFREY NNKO

KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt.Moses Kusiluka amesema, Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta ya mazao ya mboga, matunda, maua na mimea mingine jumuishi (horticulture).
Ameyasema hayo leo Novemba 12,2025 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano mkubwa wa Biashara na Uwekezaji katika Kilimo cha Horticulture (HORTICULTURE BUSSINES AND INVESTIMENT SUMMIT-HoBIS 2025) unaowakutanisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi.

Lengo la mkutano huo wa siku mbili kuanzia Novemba 12 hadi 13,2025 ni kujadili fursa, changamoto na mikakati ya kukuza sekta hiyo nchini.

“Soko la Dunia linabadilika kwa kasi, hivyo ni lazima tuwe wabunifu,wenye ubora na wenye kuaminika.HoBIS2025 si jukwaa la mijadala tu, bali ni jukwaa la utekelezaji na Serikali iko tayari kusimamia matokeo yake."
Dkt.Kusilukwa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi huo, amewakilishwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu),Dkt.Jimy Yonazi.

Amesema, mafanikio hayo yamechagizwa kwa kiasi kikubwa na jitihada za Asasi Kilele ya Sekta Binafsi inayoendeleza na kukuza Sekta ya Horticulture nchini (TAHA).
Balozi Dkt.Kusilukwa amesema, uzalishaji wa mazao hayo umeongeza kutoka tani milioni 1.1 mwaka 2003/04 hadi zaidi ya tani milioni 8.4 mwaka 2023/24.

Vilevile, amefafanua kuwa, mauzo ya nje yameongezeka kutoka dola za Kimarekani milioni 64 hadi zaidi ya dola za Kimarekani milioni 569 katika kipindi hicho.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali ya imejipanga kuifanya sekta ya horticulture kuwa injini ya mageuzi ya kiuchumi nchini kupitia sera shirikishi,jumuishi na uwekezaji katika miundombinu.

Pia,amesema ushirikiano wa sekta binafsi na umma katika sekta hii unaendelea kukua kwa kasi na kuvutia wawekezaji zaidi nchini.

Ameongeza kuwa, kuanzishwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) ni miongoni mwa hatua zilizosaidia kurahisisha usimamizi na maendeleo ya sekta hiyo.

Katika hatua nyingine amesema, Serikali imeboresha sera za kodi na biashara, kuimarisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), ujenzi wa maghala ya baridi, maboresho ya bandari na viwanja vya ndege yote hayo ni ishara ya dhamira ya dhati ya Serikali kuikuza horticulture kama nguzo ya ajira, kipato na uchumi wa taifa.
Amesema, hatua hizo zimeongeza ufanisi wa uzalishaji na usafirishaji wa mazao ya horticulture kwenda masoko ya nje.

Mbali na hayo amesema,juhudi hizo zinaendana na Mpango Mkuu wa Kilimo 2050 na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) ambapo horticulture imepewa kipaumbele kama kichocheo cha ajira na ukuaji wa viwanda vya kusindika mazao nchini.

Kiongozi huyo amewataka wadau wa sekta hiyo kushirikiana kwa vitendo katika kukuza ubora wa bidhaa na kufuata viwango vya kimataifa ili Tanzania iweze kushindana kimataifa kwa ubora na uaminifu zaidi.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli amesema, sekta hiyo imerekodi mafanikio makubwa kutokana na sera madhubuti za serikali,uwekezaji wa kimkakati na ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi na washirika wa maendeleo.

Mweli amewataka washiriki kuweka mikakati ya pamoja itakayohakikisha sekta ya horticulture inakuwa chachu ya uchumi jumuishi, ubunifu na maendeleo endelevu kwa Watanzania wote nchini.

Amesisitiza kuwa, sekta hiyo imeendelea kuwa chanzo muhimu cha mapato kwa wakulima na Taifa kwa ujumla, kutokana na mchango wake katika Pato la Taifa na upatikanaji wa fedha za kigeni.
Pia,amebainisha kuwa kupitia ushirikiano huo, masoko zaidi ya tisa yamefunguliwa, uwekezaji umeongezeka, na makampuni binafsi yameanzishwa kwa ajili ya kutoa ithibati za viwango akitolea mfano kampuni ya GREENCERT ambayo ni kampuni tanzu ya TAHA.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TAHA,Dkt. Jacqueline Mkindi amesema, dhamira ya taasisi hiyo ni kuhakikisha thamani ya mazao ya horticulture inapaa zaidi ili wakulima waweze kunufaika vilivyo kutokana na uzalishaji wao.

Dkt.Mkindi ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa ushirikiano mkubwa inaoutoa katika kuhakikisha sekta ya horticulture inaendelea kukua na kuchangia kikamilifu katika uchumi wa taifa.

Mkutano huu wa kwanza na wa aina yake unawapa wadau fursa ya kujadili sera, teknolojia,kushirikiana fursa za masoko, pamoja na miundombinu inayohitajika ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya mboga na matunda nchini.

Katika hatua nyingine, Mkutano wa Kimataifa wa Horti Logistica Africa umezinduliwa rasmi leo.

Uzinduzi huo umefanywa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi, akimwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi, na unatarajiwa kufanyika kila mwaka mwezi Novemba, ukileta pamoja wadau wa sekta ya horticulture kutoka ndani na nje ya Afrika.

Baraza hili litakuwa jukwaa muhimu la kujadili mafanikio, changamoto na fursa za kukuza tasnia ya horticulture kuanzia shambani hadi sokoni.
Kupitia ushirikiano wa Serikali na TAHA, Mkutano huu wa Horti Logistica Africa umezinduliwa rasmi jijini Dar es Salaam likiwa ni jukwaa jipya litakalowakutanisha wadau wa horticulture Afrika nzima kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga ushirikiano wa kimataifa.

Aidha, Serikali imeahidi kuendelea kuimarisha sera, miundombinu ya uhifadhi, usafirishaji na masoko ili kuendeleza sekta hii inayotoa ajira kwa maelfu ya vijana na wanawake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news