Usajili wa VICOBA ni silaha dhidi ya umaskini-BoT

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa, mtu au kikundi cha watu ambacho kitatoa huduma ndogo za fedha daraja la nne (VICOBA) kwa kukusanya na kupokea michango ya wanachama bila usajili wa Serikali kitakuwa kinavunja sheria.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 20,2025 na Meneja wa Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Bw.Dickson Gama wakati akiwasilisha mada ya elimu kuhusu huduma ndogo za fedha na usajili wa vikundi.

Ni katika siku ya pili ya semina kwa waandishi wa habari za uchumi na biashara nchini ambayo imeratibiwa na BoT jijini Dodoma huku ikiwakutanisha washiriki kutoka Zanzibar, Dodoma, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

"Kwa wale ambao wanaendesha VICOBA bila kusajiliwa ni kosa kisheria, na sheria imeweka adhabu kali, adhabu yake ni faini ya shilingi milioni 1 hadi 10 na adhabu ya kifungo cha miaka miwili hadi miaka mitano au vyote kwa pamoja."

Amesema, hadi kufikia Septemba,mwaka huu jumla ya vikundi vya kijamii 70,800 vilikuwa vimesajiliwa nchini, ambapo usajili unafanyika kupitia Wezesha Portal na Ofisi ya Rais-TAMISEMI ndiyo imekasimiwa majukumu ya kusimamia hilo.

Kupitia jukwaa hilo la kidijitali, OR-TAMISEMI inawajibika kupokea maombi ya vikundi na kuyachakata kwa hatua zaidi.

Bw.Gama amesema,usajili wa vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha ni utekelezaji wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya 2018 inayolenga kuhakikisha kuwa sekta ya huduma ndogo za fedha inasimamiwa vizuri.

Pia,ni ili iweze kuwa imara na kuchangia juhudi za Serikali za kuongeza upatikanaji wa huduma za fedha na kupunguza kiwango cha umaskini katika jamii ya Watanzania.
Amesema, ni vyema wananchi wakaendelea kusajili vikundi vyao vya huduma ndogo za fedha kupitia mfumo wa Wezesha Portal ambayo ni njia rahisi na haina gharama yoyote na inaokoa muda.

"Huduma Ndogo za Fedha zina mchango mkubwa katika kuwezesha wananchi kuongeza kipato,kusaidia makundi maalum na wale ambao walikuwa hawapati huduma ndogo za fedha, hivyo kupunguza au kuwaondolea umaskini."

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kutosita kutoa taarifa kuhusu mtu au watu ambao wanaendesha vikundi vya kijamii bila usajili, pia amesema wanaendelea kutoa elimu kwa umma ili kuwapa uelewa wa kutosha.

"Lengo na nia ya Serikali kupitia Benki Kuu ni kuhakikisha kunakuwa na ulinzi na usalama kwa hawa watoa huduma ndogo za fedha kule wanakotoa huduma ndogo za fedha daraja la nne."

Bw.Gama amesema kuwa, jitihada hizi za Serikali zimewezesha ustawi na uendelevu wa huduma ndogo za fedha daraja la nne huku kesi za watu kupoteza fedha zao zikiwa zimepungua.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here