ZANZIBAR-Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Zanzibar, Mheshimiwa Anna Atanasi amezindua Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake na Wasichana inayoanza leo Novemba 25 hadi Desemba 10,2025.
Wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa wizara hiyo uliopo Kinazini, Waziri Atanasi amewaeleza wahariri na waandishi wa habari kuwa, kwa mwaka huu itaongozwa na kaulimbiu ya Mitandao Salama ni Haki:Maliza Ukatili wa Kimtandao kwa Wanawake na Watoto."Kaulimbiu hii inaakisi changamoto mpya zinazoongezeka kwenye majukwaa ya kidijitali. Ukatili wa kimtandao umekuwa ukiathiri kwa kiwango kikubwa wanawake na watoto, ikiwemo kudhalilishwa, kusambaziwa taarifa binafsi bila ridhaa, kurubuniwa, na vitisho vinavyoathiri afya ya akili, utu na usalama wao."

Amesema,maadhimisho ya siku 16 huwa yanafanyika kila ifikapo tarehe 25 Novemba 2025 hadi 10 Disemba 2025 kwa shughuli mbalimbali nchini.
Waziri huyo amebainisha kuwa,shughuli hizo huwa zinalenga kukabiliana na tatizo la ukatili na udhalilishaji.
Aidha, amesema kwa kipindi cha mwaka 2023 jumla ya matukio 1,954 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa, mwaka 2024 matukio 1,809 na mwaka 2025 kuanzia Januari hadi Oktoba 2025 jumla ya matukio 1,022 yameripotiwa.
"Katika matukio yote hayo waathirika wakuu ni wanawake na watoto. Aidha, watoto wa kike na wakiume wamekua ndio waathirika wakubwa zaidi wa matokeo hayo ya ukatili na udhalilishaji."
Vilevile amesema, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia wizara hiyo imejiwekea vipaumbele vya kukabiliana na tatizo la vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji wa Wanawake na Watoto (GBV/VAC).
"Tunaimarisha sera na sheria, tunaimarisha Vituo vya Mkono kwa Mkono (One Stop Centers), tunajenga uwezo wa maafisa ustawi, walimu, polisi na wadau wengine, tunahamasisha jamii kuhusu matumizi salama ya mitandao, na tunashirikiana na wadau wa kimataifa kama UN Women, UNICEF, na UNFPA katika kutekeleza programu za ulinzi wa wanawake na watoto."
Aidha, amesema kwa mwaka 2025 katika kipindi cha kampeni za siku 16 wizara imepanga kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu kupitia vyombo vya habari, kutoa huduma za ushauri na upatikanaji wa haki kwa wahanga wa masuala ya udhalilishaji kwenye mikoa yote mitano ya Unguja na Pemba.
Pia,kujenga uelewa wa wandishi katika kuripoti na kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kuripoti na athari za matumizi mabaya ya mitandao, na kuimarisha maudhui ya upatikanaji wa haki na ustawi wa jamii kwa kupitia vyombo vya sheria na kutunga sera.
"Ndugu waandishi wa habari,mna nafasi muhimu katika kufikisha ujumbe sahihi kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia na kuhamasisha jamii kulinda haki za wanawake na watoto.
"Tunawaomba muendelee kufanya kazi kwa weledi, kuzingatia maadili ya taaluma, na kuhakikisha habari zenu zinasaidia kujenga jamii isiyo na ubaguzi wala ukatili."
Mbali na hayo, Waziri huyo ametoa wito kwa wananchi wote wa Zanzibar kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanalinda wanawake, watoto na familia.
Amesema,ukatili sio utamaduni wetu, na ulinzi wa haki za binadamu ni wajibu wetu wa pamoja.
Waziri Atanasi amesema,mitandao salama ni haki ya kila mmoja na tunapaswa kuhakikisha hakuna anayebaguliwa au kuumizwa kupitia mitandao au katika maisha ya kila siku.
"Tukishikanama na kuwajibika inawezekana kuondoa tatizo la ukatili na udhalilishaji Zanzibar."
Wakati huo huo, Waziri Atanasi amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi, kwa kumuamini na kumteua kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto.





