ARUSHA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeratibu Mkutano wa Kamati ya Ufundi ya Uhasibu na Fedha, uliowakutanisha wataalamu kutoka benki kuu za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa ajili ya kujadili maendeleo, changamoto na mustakabali wa fedha endelevu katika ukanda huo.
Mkutano huo umefanyika jijini Arusha kuanzia Desemba 1 hadi 4, 2025, na ulizinduliwa rasmi na Meneja wa Idara ya Uchumi wa BoT–Tawi la Arusha, Bw. Aristedes Mrema, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa tawi hilo.
Akifungua mkutano huo, Bw. Mrema alisema kuwa ni hatua muhimu katika safari ya kuijenga jumuiya yenye dira ya pamoja katika kusimamia mifumo ya fedha iliyo thabiti, shindani na endelevu.
Katika kipindi cha siku nne, washiriki walijadili mada mbalimbali zinazohusu mustakabali wa sekta ya fedha, zikiwemo nafasi ya uhasibu katika ununuzi wa dhahabu ya fedha (Monetary Gold), matumizi ya Akili Unde (AI) katika uchanganuzi na usimamizi wa data za sekta ya fedha, pamoja na mbinu bora za kufanya tathmini za uendelevu zinazozingatia viwango vya kimataifa vya kuripoti na kusimamia taasisi za fedha.
Kupitia majadiliano hayo, mkutano umeimarisha msingi wa ushirikiano wa kikanda katika masuala ya usimamizi wa fedha na kuonesha dhamira ya Benki Kuu ya Tanzania kuongoza mageuzi yanayolenga kukuza uthabiti, uwazi na uendelevu wa mifumo ya fedha ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.



