ARUSHA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha mafunzo maalum kwa wanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Fedha na Benki kutoka Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), kwa lengo la kuongeza uelewa wao kuhusu masuala muhimu ya sekta ya fedha na kuwapa mtazamo wa moja kwa moja kuhusu namna tasnia hiyo inavyofanya kazi.
Mafunzo hayo, yaliyofanyika Alhamisi, Desemba 4, 2025, yalijumuisha mada mbalimbali kuhusu usimamizi wa taasisi za fedha, ikiwemo mabenki, pamoja na elimu juu ya uwekezaji katika dhamana za Serikali.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Meneja Msaidizi wa Usimamizi wa Mabenki Makubwa, Bw. Naiman Juwael, alisisitiza umuhimu wa mabenki kusimamiwa na kukaguliwa mara kwa mara ili kuhakikisha uthabiti wa sekta ya fedha unaendelea kuimarika.
Alieleza kuwa usimamizi madhubuti wa mabenki ni msingi muhimu katika kulinda uchumi wa nchi na maslahi ya wananchi.
Mafunzo haya ni sehemu ya jitihada endelevu za BoT katika kuwafikia wadau wake, hususan taasisi za elimu ya juu, kwa lengo la kuongeza ufahamu kuhusu majukumu yake, kukuza uelewa wa wanafunzi kuhusu masuala ya kifedha, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma kati ya Benki Kuu na vyuo mbalimbali nchini.


