Bwana katusaidia

NA LWAGA MWAMBANDE

LEO Desemba 31,2025 ni siku ya mwisho kabla ya kuupokea mwaka mpya 2026. Kwa ujumla, tunaungana kumshukuru Mungu kwa kutuvusha salama katika mwaka 2025, mwaka uliodhihirika kwa baraka, ulinzi na neema zake.
Katika kipindi chote cha mwaka, Watanzania tumeshuhudia mkono wa Mungu ukiendelea kutuongoza, kuimarisha imani, na kutoa nguvu katika nyakati za changamoto, hali iliyoendeleza matumaini na mshikamano katika jamii zetu.

Tunapoelekea mwaka 2026, ni maombi yangu, Mungu azidi kuubariki mwaka mpya kuwa wa amani, afya njema na maendeleo ya kiroho na kijamii.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anabainisha kuwa, tunaingia mwaka 2026 kwa imani thabiti, tukimuamini Mungu kuongoza hatua zote, kuimarisha maadili na kuijaza mioyo ya watu upendo, unyenyekevu na shukrani, kwa lengo la kujenga jamii na taifa lenye hofu ya Mungu na ustawi endelevu. Endelea;

1. Bwana katusaidia,
Uhai katulindia,
Ibilisi litujia,
Kaaibika mwenyewe.

2. Bwana katusaidia,
Magonjwa katushindia,
Shetani litutumia,
Kaaibika mwenyewe.

3. Bwana katusaidia,
Watoto katulindia,
Aliyewashambulia,
Kaaibika mwenyewe.

4. Bwana katusaidia,
Njaa lipotujia,
Yule alitubania,
Kaaibika mwenyewe.

5. Bwana katusaidia,
Maombi litusikia,
Ibilisi lizuia,
Kaaibika mwenyewe.

6. Bwana katusaidia,
Afya ametupatia,
Mwovu livyotupania,
Kaaibika mwenyewe.

7. Bwana katusaidia,
Shule tumejishindia,
Tego liyetufanyia,
Kaaibika mwenyewe.

8. Bwana katusaidia,
Ebeneza twamwimbia,
Baya liyetufanyia,
Kaaibika mwenyewe.

9. Bwana katusaidia,
Mwaka tunamalizia,
Lotaka tufanyizia,
Kaaibika mwenyewe.

10. Bwana katusaidia,
Mwaka mpya twaingia,
Mtu liyetuwangia,
Kaaibika mwenyewe.

11. Bwana katusaidia,
Kinga ametufanyia,
Alotaka jipigia,
Kaaibika mwenyewe.

12. Bwana katusaidia,
Amani katupatia,
Lodhani tutaishia,
Kaaibika mwenyewe.

13. Bwana katusaidia,
Ni mengi katushindia,
Kwamba tutaangamia,
Kaaibika mwenyewe.

14. Bwana katusaidia,
Yeye kwetu ndiye njia,
Sumu alotumwagia,
Kaaibika mwenyewe.

15. Bwana katusaidia,
Nasi tutamuishia,
Mwovu huko kasalia,
Kaaibika mwenyewe.

16. Bwana katusaidia,
Baraka atutakia,
Laana alopania,
Kaaibika mwenyewe.

17. Mabaya yalitujia,
Na kwa kweli tulilia,
Wanyonge tukabakia,
Shukrani kwa mwenyewe.

18. Kote katusaidia,
Hata kutukumbatia,
Wameenda twasalia,
Shukrani kwa mwenyewe.
(1 Samweli 7:12)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news