Serikali imeanza rasmi utekelezaji wa mpango wa ufadhili wa Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Takwimu, Akili Unde (AI) na Sayansi Shirikishi chini ya Samia Scholarship Extended (SSE DS/AI+), hatua inayolenga kuimarisha rasilimali watu katika sekta ya sayansi na teknolojia nchini.
Katika awamu ya kwanza, wanafunzi 10 wamepatiwa ufadhili huo na watajiunga na masomo katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, huku wengine 10 wakitarajiwa kuanza masomo yao katika Indian Institute of Technology Madras Zanzibar Campus.
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 25, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema uwekezaji huo ni mkakati wa Serikali kukidhi ongezeko la mahitaji ya wataalamu wa takwimu, akili unde na teknolojia bunifu.
Amebainisha kuwa jumla ya Sh bilioni 5 zimetengwa kugharamia mpango huo, akisisitiza kuwa ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kujenga uchumi wa maarifa unaotegemea sayansi na ubunifu.
Prof. Mkenda ametoa wito kwa wadau kushirikiana na Serikali kwa kuchangia mfuko wa Samia Scholarship, huku akiwataka wanafunzi waliopata ufadhili wa Shahada ya Kwanza kupitia mpango huo kuangalia majina yao kwenye tovuti za Wizara, Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania pamoja na Taasisi ya Nelson Mandela.
Tags
Kurasa za Magazeti
Kurasa za Mbele na Nyuma za Magazeti
Magazeti
Magazeti ya Leo
Magazetini
Magazetini leo
Yaliyojiri Magazetini Leo


















