DAR-Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Camillus Wambura, amefungua rasmi mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Sekretarieti ya Maadili ya Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dodoma, yanayofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (DPA) kuanzia tarehe 15 hadi 19 Disemba, 2025.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, IGP Wambura alisisitiza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha watendaji kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uwajibikaji na uadilifu mkubwa zaidi ili kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii.

Alibainisha kuwa, mafunzo hayo yataimarisha uwezo wa washiriki katika kusimamia maadili, kushughulikia malalamiko ya wananchi, kuandaa taarifa za robo mwaka na mwaka pamoja na kutumia kikamilifu Mfumo wa Kielektroniki wa Kushughulikia Mrejesho (e-Mrejesho) ili kuongeza uwazi na ufanisi ndani ya Jeshi la Polisi.
Akihitimisha hotuba yake, IGP Wambura aliwataka washiriki kuzingatia kikamilifu yale watakayofundishwa kwani mada zitakazowasilishwa kwao zitawawezesha kwenda kutambua na kutekeleza kikamilifu majukumu ya Kamati ya Kusimamia Maadili na Ushughulikiaji wa Malalamiko ya wananchi.
Kwa upande wake, Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu wa Jeshi la Polisi, CP Tatu Jumbe, akizungumza wakati wa kumkaribisha IGP Wambura kufungua mafunzo hayo, alisema mafunzo mafunzo hayo yanafanyika ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Tume ya Haki Jinai.
Sambamba na maazimio yaliyotokana na Semina Elekezi ya Maafisa Waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Taasisi zilizo chini yake iliyofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro Septemba 2024, akiongeza kuwa mafunzo hayo yatakuwa endelevu ili kuimarisha ufanisi na weledi katika utekelezaji wa majukumu yake.
Tags
Habari
IJP Camillus Wambura
Jeshi la Polisi Tanzania
Maadili
Uwajibikaji
Viongozi Jeshi la Polisi






