MWANZA-Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limeendesha operesheni maalumu ya msako na doria katika maeneo ya milima na mapango yanayotajwa kuwa maficho ya wahalifu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutokomeza uhalifu mkoani humo.
Akizungumza wakati wa doria hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, amesema operesheni hiyo ilianza rasmi Novemba 29, 2025 ikihusisha maeneo ya Kata za Mkolani, Buhongwa, Isamilo, Mhandu, Igoma Kati na Mahina Wilaya ya Nyamagana pamoja na Kitangili, Bwiru Ziwani, Kawekamo na Ibungilo, Wilaya ya Ilemela.
Aidha,Kamanda Mutafungwa amesema jumla ya watuhumiwa 12 wamekamatwa wakiwa wamejificha katika mapango hayo huku wakiwa na vifurushi vya bangi na kuongeza kuwa wanaendelea kuhojiwa na watafikishwa kwenye vyombo vya sheria baada ya upelelezi kukamilika.

Pia amesema, operesheni hiyo ni endelevu na Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha ulinzi na usalama vinadumishwa katika Mkoa wa Mwanza.
Sambamba na hayo Kamanda Mutafungwa ametoa wito kwa wakazi wa maeneo ya milimani, misituni na jirani na mapango kutoa taarifa mapema endapo watabaini uwepo wa watu wasiowafahamu au wanyama wakali ili hatua zichukuliwe mara moja.
Kwa upande wake Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kasese, Gaudence Mtepa, ameipongeza operesheni hiyo na kutoa ombi kwa Jeshi la Polisi kusaidia kulipua baadhi ya maeneo ya milima yanayotumika mara kwa mara na wahalifu kama maficho baada ya kutekeleza matukio ya uhalifu katika mitaa jirani.Jeshi la Polisi limetoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana kwa karibu na vyombo vya dola katika juhudi za kuhakikisha Mkoa wa Mwanza unabaki kuwa salama kwa watu na mali zao.
