Magari yaliyotumika kusafirishia mwili wa marehemu yachomwa moto Morogoro

MOROGORO-Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limetoa taarifa ya kuchomwa moto na kuharibiwa kwa magari mawili yaliyotumika kusafirishia mwili wa marehemu, tukio lililofanywa na waombolezaji wa msiba baada ya kutilia mashaka mazingira ya kifo cha marehemu.
Taarifa ya Desemba 18, 2025 iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama imeeleza kuwa, tuukio hilo limetokea Desemba 17, 2025 katika kitongoji cha Kilingeni, kijiji cha Lusanga, kata ya Diongoya, tarafa ya Turiani, wilaya ya Mvomero, ambapo magari namba T. 214 EJU aina ya Mazda CX-5 na T. 350 DCH aina ya Toyota Noah yalichomwa moto na kuharibika.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa magari hayo yalitumika kusafirisha mwili wa marehemu Mwanahasan Juma Hamis (18) mfanyakazi wa kazi za ndani mkazi wa Turiani aliyefariki kwa maradhi jjijni Dar es Salaam kisha kusafirishwa kwenda mkoani Morogoro kwa shughuli za mazishi.

“Wakati taratibu za mazishi zikiandaliwa ilitokea taharuki iliyohusishwa na kutiliwa mashaka ya mazingira ya kifo cha marehemu hali iliyosababisha kuchomwa kwa magari hayo na kuwafungia ndani wasindikizaji wa msiba ili watoe maelezo zaidi,”imesema sehemu ya taarifa hiyo.

“Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na uongozi wa serikali ya mtaa waliweza kuwaokoa wasindikizaji wa msiba waliofungiwa na kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusu mazingira ya kifo hicho ambapo taarifa kamili itatolewa baadae.”

Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limesema linaendelea kuimarisha usalama katika eneo hilo na kuwataka wananchi kuacha utamaduni wa kujichukulia sheria mkononi na kusisitiza kuwa utamaduni huo ni kinyume cha sheria na una madhara makubwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here