MBUNGE wa Jimbo la Mtumba na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amemkabidhi nyumba iliyofanyiwa ukarabati Bi. Verian Mlewa mwenye umri wa miaka 75, mkazi wa Kata ya Mtumba jijini Dodoma, ambaye alikuwa katika hatua ya kuiuza nyumba yake kwa Shilingi 500,000 ili kupata fedha za matibabu baada ya kuugua uvimbe katika ubavu.
Hatua hiyo imefuatia taarifa za hali ya bibi huyo kuripotiwa kwenye vyombo vya habari, ambapo kwa kushirikiana na Kitengo cha Ustawi wa Jamii, Bi. Verian alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na kufanyiwa upasuaji uliomwezesha kurejea katika hali nzuri ya afya.
Akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Vikonje B, Kata ya Mtumba, wakati wa kukabidhi nyumba hiyo Desemba 26, 2025, Mhe. Mavunde amesema kuwa aliguswa na simulizi ya maisha ya bibi huyo baada ya kuona taarifa zake kwenye vyombo vya habari.
“Nimeona nitumie fursa hii kuikabidhi nyumba iliyofanyiwa ukarabati. Nyumba hii ni ya Bi. Verian aliyeijenga mwenyewe. Baada ya kuona taarifa kuwa anaumwa na kukosa fedha za matibabu hadi kufikia hatua ya kutaka kuuza nyumba yake, tulishirikiana na ofisi ya ustawi wa jamii kumpeleka hospitalini, akafanyiwa upasuaji na kupona,” amesema Mhe.Mavunde.
Tags
Kurasa za Magazeti
Kurasa za Mbele na Nyuma za Magazeti
Magazeti
Magazeti ya Leo
Magazetini
Magazetini leo
Yaliyojiri Magazetini Leo














