ZANZIBAR-Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga amesema,Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST) ni muhimili muhimu katika kutoa mafunzo ya sayansi, ufundi na teknolojia nchini, hatua inayochangia kuinua uchumi na maendeleo ya taifa.

Ameyasema hayo katika Mahafali ya 11 ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST) yaliyofanyika katika viwanja vya taasisi hiyo, Mbweni, Wilaya ya Magharibi B, ambapo amesema kuwa KIST imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu ya ufundi katika ngazi mbalimbali ikiwemo shahada ya kwanza, stashahada na astashahada.
Amesema kuwa,taasisi hiyo ni miongoni mwa taasisi muhimu zinazotoa taaluma zinazochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi kupitia sayansi, teknolojia, ufundi na ubunifu.
Mhe. Soraga ameongeza kuwa mahafali ni fursa muhimu ya kutathmini mafanikio ya taasisi za elimu katika kutekeleza majukumu yao ya msingi ya kutoa elimu na ujuzi, hivyo ameipongeza KIST kwa mafanikio iliyoyapata na kuitaka kuendelea kuyaimarisha ili kuandaa vijana kitaaluma kwa viwango mbalimbali vinavyokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Aidha, ameupongeza uongozi wa Baraza la Taasisi, wakufunzi, wafanyakazi pamoja na wadau kwa kuendelea kuisimamia na kuiunga mkono taasisi hiyo katika azma yake ya kutoa elimu bora yenye ujuzi, pamoja na kuwajengea wahitimu uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa kupitia mabadiliko ya kidijitali na maendeleo ya teknolojia.
Ameongeza kuwa wahitimu wanapaswa kuzingatia nidhamu, kutojiridhisha na elimu waliyoipata na kuendelea kuongeza juhudi za kujiongezea maarifa ili kuchangia kikamilifu katika kukuza uchumi wa nchi kupitia taaluma na ubunifu.
“Leo ni siku ya furaha, fahari na kumbukumbu kwenu. Mmeonesha juhudi, nidhamu na bidii katika safari yenu ya kitaaluma na hatimaye mmefanikiwa kuhitimu. Hongereni sana kwa hatua hii,” alisema Mhe. Soraga.
Hata hivyo, amesema taifa limeongeza idadi ya wataalamu ambao ni chachu ya maendeleo, hivyo amewataka wahitimu kutumia taaluma walizopata kuleta mabadiliko chanya yenye tija na manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume, Dkt. Afua Khalfan Mohamed, amesema taasisi hiyo ina dhamira ya kuandaa wataalamu na wabunifu wenye ujuzi wa vitendo, maadili mema na uwezo wa kujiajiri na kuajiri wengine.
Amesema kuwa, maendeleo ya dunia yanategemea kwa kiasi kikubwa sayansi na teknolojia, hali iliyosababisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuziweka sekta hizo katika vipaumbele vyake kupitia miongozo mikuu ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020-2050.
Amefafanua kuwa,Baraza la Taasisi litaendelea kusimamia sera, mikakati na uwekezaji unaolenga kuboresha ubora wa elimu ya ufundi na teknolojia, miundombinu, utafiti, ubunifu pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi, sekta binafsi na viwanda ili kuhakikisha wahitimu wanapata elimu inayokidhi viwango vya ajira.
Aidha, amewahimiza wahitimu kuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo na kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi kupitia matumizi ya sayansi na teknolojia.
Naye Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume, Dkt. Mahmoud Abdulwahab Alawi, ameiomba Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu kuimarisha ushirikiano na taasisi hiyo ili kuendelea kulea na kuibua vipaji katika sekta ya sayansi na teknolojia.Amesema ushirikiano huo utafungua fursa zaidi kwa taasisi, wakufunzi na wanafunzi na kuchangia maendeleo ya haraka ya sekta ya sayansi na teknolojia nchini.
Ameeleza kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana, taasisi hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya ongezeko la idadi ya wanafunzi katika fani za teknolojia, ubunifu na ujasiriamali wa kidijitali, hali inayoongeza mahitaji ya vifaa vya kisasa vya kufundishia ili kukuza ubunifu.
Katika mahafali hayo, wahitimu wa kada mbalimbali za mafunzo ya amali katika ngazi ya astashahada, stashahada na shahada walitunukiwa vyeti vyao.
Tags
Habari
Karume Institute of Science and Technology
Sekta ya Elimu Zanzibar
Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST)
Zanzibar News
















