Watumishi wa Umma wasimamishwa kazi

PWANI-Watumishi wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, ambao ni Mkuu wa Idara ya Fedha na Afisa Utumishi na Rasilimali Watu, wamesimamishwa kazi kufuatia tuhuma za usimamizi dhaifu wa fedha za miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani humo.
Hatua hiyo imeelekezwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Mhe. Reuben Kwagilwa, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, OWM–TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Mafia.
Mhe. Kwagilwa amesema hajaridhishwa na namna fedha za miradi zinavyosimamiwa pamoja na utekelezaji wake, akieleza kuwa tangu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, Serikali imepeleka zaidi ya shilingi Bilioni 24 wilayani Mafia kwa ajili ya miradi ya maendeleo, fedha ambazo zinapaswa kusimamiwa kwa uadilifu na uwajibikaji wa hali ya juu.

“Sijaridhishwa na usimamizi na utekelezaji wa miradi unaoendelea. Tangu Rais Samia aingie madarakani, ameleta fedha zaidi ya shilingi bilioni 24 hapa Mafia, lakini bado kuna watu hawazisimamii ipasavyo,” amesema Mhe. Kwagilwa.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amemuagiza Katibu Mkuu, OWM–TAMISEMI kutuma timu maalumu kufuatilia mwenendo wa Afisa Utumishi na Rasilimali Watu wa halmashauri hiyo ili kubaini uzingatiaji wa taratibu za kiutumishi.

Aidha, amemtaka Katibu Mkuu kuhakikisha ndani ya siku 21 anapeleka Mkuu wa Idara ya Ujenzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mafia ili miradi ya maendeleo ipate usimamizi wa karibu na kuepusha ucheleweshaji wa miradi na matumizi yasiyo sahihi ya fedha za miradi hususani ujenzi wa miundombinu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news