NA LWAGA MWAMBANDE
VIKUNDI vya Village Community Banks (VICOBA) vinaendelea kuonesha mchango mkubwa katika kuwawezesha wanawake kiuchumi na kijamii, hususan katika jamii za kipato cha chini mijini na vijijini.

Aidha, kupitia mfumo wa akiba na mikopo, wanawake wengi wamefanikiwa kuboresha maisha yao, kukuza biashara ndogo ndogo na kuchangia maendeleo ya familia zao.
VICOBA ni mfumo wa kifedha wa kijamii unaowawezesha wanachama kuweka akiba kidogo kidogo na kukopeshana kwa masharti nafuu, tofauti na taasisi kubwa za kifedha.
Wanawake wamekuwa walengwa wakuu wa mfumo huu kutokana na nafasi yao katika uendeshaji wa kaya na shughuli ndogo za uzalishaji mali.
Kupitia VICOBA, wanawake wengi wamepata fursa ya kupata mitaji ya kuanzisha na kukuza biashara kama vile ujasiriamali wa chakula, kilimo cha bustani,ushonaji,biashara ndogo ndogo,kujenga na hata kusomesha.
Akiba na mikopo inayotolewa imechangia kuongeza kipato cha kaya na kupunguza utegemezi wa kifedha kwa wanawake.
Katika maeneo mengi nchini, huu ni msimu wa wanawake kuvunja VICOBA vyao, kwa kuliona hilo mshairi wa kisasa ana jambo kidogo kuhusu wababa.Endelea;
1. Umekwishashitukiwa, unavyojipendekeza,
Wajua kafanikiwa, mifuko anaijaza,
Unataka tambuliwa, nawe aweze kujaza,
Mama kivunja vikoba, wababa mwajisogeza.
2. Kazi zote za nyumbani, baba unazichakaza,
Mama akija njiani, kwa karibu wampoza,
Kama maji mtungini, jinsi unajilegeza,
Mama kivunja vikoba, wababa mwajisogeza.
3. Vurugu vurugu zote, za mama kumuumiza,
Sasa zinakwisha zote, asije kutelekeza,
Upole ni kama wote, kila kitu wapongeza,
Mama kivunja vikoba, wababa mwajisogeza.
4. Yale mahitaji yako, wafanya kujiongeza,
Wajisemea kivyako, kwa sauti ya kuweza,
Ili huyo mwenzi wako, aweze kukusikiza,
Mama kivunja vikoba, wababa mwajisogeza.
5. Wamama kuwa makini, msije kujilegeza,
Panga bajeti makini, mahitaji kutimiza,
Masazo yale mwishoni, muweze kujipongeza,
Mama kivunja vikoba, wababa, mwajisogeza.
6. Huu upendo wa sasa, bora kuuendeleza,
Muda wa kuchanga pesa, vikoba kudunduliza,
Hiyo kwa mama hamasa, asijekutelekeza,
Mama kivunja vikoba, wababa mwajisogeza.
7. Wamama mnatubeba, hili ninawaeleza,
Kwa hivyo vyenu vikoba, mahitaji twatimiza,
Sherehe zinavyokaba, ada mnazimaliza,
Mama kivunja vikoba, wababa mwajisogeza.
8. Upendo kwenye vikoba, usiwe mauzauza,
Endelezeni wababa, muda wote kueneza,
Haba mjaze kibaba, maisha kuendeleza,
Mama kivunja vikoba, wababa mwajisogeza.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602