DODOMA-Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel M. Maneno amemuwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari katika sherehe za kupokelewa na kukubaliwa Mawakili wapya wa Kujitegemea zilizofanyika tarehe 5 Desemba, 2025 jijini Dodoma.

Akizungumza katika sherehe hizo za kuwapokea na kuwakubali Mawakili wapya wa Kujitegemea, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewakumbusha Mawakili hao kuwa wana nafasi kubwa katika kuondoa changamoto za Kisheria zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
"Naomba nitumie siku hii adhimu kuwaelezea Mawakili wapya kuwa, mna nafasi kubwa sana ya kuondoa changamoto mbalimbali za kisheria katika Taifa hili,"amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewakumbusha Mawakili wa Serikali juu ya umuhimu wa kuzingatia weledi katika utendaji wa haki kwa wananchi, ambapo ameeleza kuwa Mawakili ni kiungo muhimu sana baina ya wananchi na Mahakama katika kuichambua na kuitafsiri haki na sheria.
"Nitumie nafasi hii kuwaeleza Mawakili mliokubaliwa leo kuwa, mna nafasi kubwa katika kuhakikisha jukumu la utoaji haki linatekelezwa kwa ufanisi na Mahakama. Mnapaswa kuisaidia Mahakama itende haki na kuhakikisha wananchi wanapatiwa haki zao wanapokwenda mahakamani au kwenye vyombo vingine vya kisheria,"amesema Mhe. Maneno.
Katika hatua nyingine, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kuunga mkono Serikali na taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za msaada wa kisheria nchini ambapo Ofisi imeanzisha Kamati za Ushauri wa Kisheria katika ngazi ya Mikoa na Wilaya pamoja na kuendesha Kliniki za msaada wa kisheria katika maeneo mbalimbali nchini.
"Napenda kuwasisitizia pia mawakili wote ikiwa ni pamoja na Mawakili mlioapishwa siku ya leo kuwa mnapaswa kushiriki katika Wiki ya Sheria na kampeni mbalimbali za kutoa misaada ya kisheria na kutoa elimu ya sheria kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini,"amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Vilevile Mhe. Maneno amewasihi Mawakili wapya kuwa nidhamu na kuzingatia Kanuni za Maadili ya taaluma ya sheria, huku akiwakumbusha kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ataendelea kudhibiti nidhamu ya Mawakili wa Kujitegemea kwa kuzingatia mamlaka aliyopewa kupitia Sheria ya Mawakili, Sura ya 341.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Jaji George M. Masaju amewataka Mawakili hao wapya waliopokelewa na kukubaliwa kufanya kazi kwa kuzingatia uadilifu kwa kufuata Katiba na Sheria za Tanzania ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa"Mnapokwenda kutekeleza majukumu yenu ni muhimu mkafanye kazi kwa uadilifu mkubwa na kuzingatia miongozo mbalimbali ikiwemo Katiba, Sheria na Kanuni mbalimbali,"amesema Jaji Mkuu.
Sambamba na hilo, Jaji Mkuu wa Tanzania amewaeleza Mawakili hao kuhakikisha wanatenda haki kwa wananchi, kwa kusimamia misingi ya sheria, kanuni na taratibu, huku wakiwa sehemu ya kuendelea kulinda amani ya Taifa.
“Niwaombe Mawakili mliokubaliwa na kupokelewa leo mkatende haki kwa wananchi, mkazingatie utawala wa sheria unafuatwa, pia ninyi ni sehemu ya kuilinda na kuitetea Amani ya Taifa hili,"amesema Jaji Mkuu.
Sherehe hizo za 73 za kuwapokea na kuwakubali mawakili wapya wa kujitegemea zimehusisha jumla ya wahitimu 774.











