Orodha ya mali zilizotaifishwa kutokana na wamiliki kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya nchini

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imefanya operesheni mbalimbali zilizofanikisha ukamataji wa jumla ya tani 3.8 za dawa za kulevya,kuteketeza ekari 18 za bangi pamoja na kutaifisha mali za wahalifu wa dawa za kulevya zenye thamani ya shilingi bilioni 3.304.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo ameyabainisha hayo leo Desemba 3,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake jijini Dar es Salaam, amesema operesheni hiyo ilifanyika Novemba,2025 huku watuhumiwa 84 wakikamatwa kuhusiana na dawa hizo.

Amesema, katika kuendeleza hatua za kukabiliana na uhalifu wa dawa za kulevya,Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ilitoa maamuzi ya kutaifishwa kwa mali zenye thamani ya shilingi bilioni 3.304 zikijumuisha nyumba,viwanja na magari.

Mali hizo, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, ni za watuhumiwa Saleh Khamis Basleman na Gawar Bachi Fakir ambao wanatuhumiwa kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Kamishna Jenerali Lyimo amefafanua kuwa,maombi ya kutaifishwa mali hizo yaliwasilishwa mahakamani hapo kutokana na uchunguzi uliofanywa na ikiabainika watuhumiwa hao wanamiliki mali ambazo zilipatikana kwa njia ya uhalifu wa biashara ya dawa za kulevya.


Amesema, utaifishaji wa mazalia ya uhalifu umewekwa kisheria ili kuifundisha jamii kuwa,uhalifu hauna faida na adhabu za kifungo hazitoshelezi kutokomeza uhalifu hasa katika makosa ya kupangwa ikiwemo makosa ya dawa za kulevya.

"Na huu ni mkakati wa kuzuia uhalifu kuendelea na kuondoa matamanio ya kufanya uhalifu,"ameongeza Kamishna Jenerali Lyimo.

Orodha ya mali zilizotaifishwa kwa mujibu wa Kamishna Jenerali Lyimo ni Apartment Namba OA2,ghorofa ya kwanza iliyopo Sea Breeze Residential Complex, kiwanja Namba 192 block 0, Jangwani Beach katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.




















Nyingine ni Apartment 6B, kiwanja Namba 26 block 52 iliyopo Kariakoo katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, nyumba iliyopo kiwanja Namba 329 na 1009 block C eneo la Mbezi katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Mali nyingine zilizotaifishwa, Kamishna Jenerali Lyimo amesema ni kiwanja Namba 69 block 7 kilichopo Kata ya Mbweni JKT katika Halmashuari ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na nyumba Namba 14 iliyopo kiwanja Namba 131 block 9 katika Mtaa wa Chui Mtoni Kijichi, NSSF House Scheme Phase III wilayani Temeke, Dar es Salaam.

Pia, amesema kuna kiwanja Namba 44768 kilichopo Mtaa wa Kigogo katika Kata ya Kisarawe II, Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam na kiwanja kilichopo Shungubweni Village Kata ya Shungubweni wilayani Mkuranga, Pwani.

Aidha, amesema kuna kiwanja Namba 53 block E kilichopo Boza Village wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani na kiwanja kilichopo Boza Village Kata ya Boza wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema,pia kuna kiwanja Namba B block C kilichopo Mtaa wa Mwambao katika Kata ya Mji Mkongwe wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Vilevile, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, kuna Apartment Namba PA1, ghorofa ya chini,Sea Breeze Residential Complex katika Kiwanja Namba 192 block P iliyopo Jangwani Beach, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Amesema, pia kuna nyumba Namba 9 iliyopo Magomeni katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam na kiwanja Namba 44746 kilichopo Mtaa wa Kigogo katika Kata ya Kisarawe II Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Kiwanja Namba 44748 kilichopo Mtaa wa Kigogo Kata ya Kisarawe II Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni na kiwanja Namba 44789 kilichopo Mtaa wa Kigogo Kata ya Kisarawe II Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.


Magari mengine, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, ni namba T 141 DKV aina ya Nissan Civilian, namba T 944 DKY aina ya Nissan Civilian, namba T 830 DLA aina ya Nissan Civilian, namba T 767 DLL aina ya Nissan Civilian, namba T 435 DJY aina ya Toyota Corrola Spacio, namba T 307 DLW aina ya Nissan Civilian na namba T 753 DKS aina ya Nissan Civilian.

Mbali na hayo, katika operesheni zilizofanyika jijini Dar es Salaam, watuhumiwa Cuthbert Kalokola (34) na Murath Abdallah (19) walikamatwa Sinza D wakiwa na vidonge 738 vya dawa mpya aina ya 3,4- Methylenedioxymethamphetamine (MDMA) vyenye uzito wa gramu 177.78, pamoja na vidonge 24 vya dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Rohypnol vyenye uzito wa gramu 10.03.

Katika eneo la Mbezi Maramba Mawili, watuhumiwa saba Jaribu Tindwa (38), Ally Meshe (39), Juma Mfamo (20), Rahim Nampanda (28), Abubakari Ally (20), Nurdin Rashid (36) na Farid Rashid (33) walikamatwa wakiwa na kilogramu 90 za dawa za kulevya aina ya skanka zilizokuwa zimefichwa ndani ya matanki ya zilizofichwa ndani ya matanki ya solar panel yaliyopakiwa kwenye basi la Falcon aina ya Scania lenye namba za usajili T372 DFK linalosafiri kati ya Tanzania na Malawi.

Vilevile, katika mpaka wa Kasesya mkoani Rukwa, Godwin Andrew (26) mkazi wa Mbalizi Mbeya alikamatwa akiwa na kilogramu 244.3 za skanka zilizofichwa ndani ya spika, mashine za kupooza hewa, mashine za kukatia majani na vifaa vya kompyuta (CPU).
Mzigo huo ulikuwa unasafirishwa kwa gari aina ya Iveco Van lenye namba za usajili za nchi ya Afrika Kusini CN 85 FN GP mali ya kampuni ya Makamua Logistics Limited.

Aidha, katika operesheni nyingine zilizofanyika mikoa mbalimbali, zilikamatwa kilogramu 2,041.45 za bangi, kilogramu 1,423.28 za mirungi, na ekari 18 za mashamba ya bangi ziliteketezwa.

Magari manne na pikipiki 12 pia vilikamatwa. Akitoa ufafanuzi kuhusu operesheni hizo, Kamishna Jenerali Lyimo alisema kuwa hatua zilizochukuliwa jijini Dar es Salaam ni sehemu ya utekelezaji wa udhibiti wa tatizo la dawa za kulevya nchi nzima.

“Operesheni hizi zinafanyika maeneo yote nchini ili kuzuia uhalifu wa dawa za kulevya na kufuta kabisa mtandao wad awa hizo,” amesisitiza Lyimo.

DCEA imetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na mamlaka hiyo kwa kutoa taarifa za uhalifu wa dawa za kulevya ili kufanikisha mapambano dhidi ya janga hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news