ARUSHA-Mkuu wa Kituo cha Polisi Utalii na Diplomasia Mkoa wa Arusha, Mrakibu wa Polisi SP Waziri Tenga amesema Kituo hicho kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji wamepanga kuanzisha kituo cha huduma kwa saa 24 chenye lengo la kuboresha na kuharakisha huduma kwa watalii na wageni.
SP Tenga ameyasema hayo leo Disemba 21, 2025 wakati alipokua anazungumza na waandishi wa habari ambapo amebainisha kuwa kituo kilichopendekezwa kitawawezesha watalii kupata huduma muhimu ikiwa ni pamoja na usaidizi kwa wale wanaopoteza hati za kusafiri kwa haraka.
Mkuu huyo wa Kituo aliendelea kufafanua kuwa kwa sababu watalii wanaingia na kutoka nchini kila wakati, kituo hicho kitakuwa kinatoa huduma kwa saa 24 kila siku bila kujali siku za sikukuu.
Katika hatua nyingine alibainisha kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo limeimarisha usalama hususani kwa watalii na wageni wanaofika mkoani humo kupitia doria mbalimbali ikiwemo za mitandaoni na maeneo wanakofikia watalii.
