Wananchi waishukuru Serikali,waiomba kuharakisha ujenzi wa barabara ya bandari kavu Kwala

PWANI-Mchambuzi wa siasa na uchumi ambaye pia ni mhubiri wa Kimataifa, Mwinjilisti Alphonce Temba leo Desemba 22, 2025, akiwa pamoja na wananchi wanaoishi pembezoni mwa Bandari Kavu ya Kwala, kutoka Kitongoji cha Ngwale kilichopo Wilaya ya Kibaha Vijijini, wameishukuru Serikali kwa ujenzi wa bandari hiyo huku wakiomba iharakishe ujenzi wa barabara inayounganisha bandari hiyo na maeneo jirani.
Barabara inayotajwa ni ile inayotoka Bandari Kavu ya Kwala kupitia Mperamumbi, Ngwale, Gwata, Chaua hadi Msola wilayani Chalinze, ambayo wananchi wanasema ni mhimili muhimu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika eneo hilo.

Wakizungumza katika mahojiano maalum yaliyofanyika karibu na Bandari Kavu ya Kwala, wananchi hao wamesema eneo hilo lina fursa nyingi za kiuchumi ambazo kwa muda mrefu hazikuweza kutumika ipasavyo kutokana na changamoto ya miundombinu.

Wamesema baadhi ya wananchi walikuwa wakitegemea shughuli zisizo endelevu kama ukataji wa mkaa na uharibifu wa misitu, hali ambayo sasa inaweza kubadilika kufuatia ujio wa bandari hiyo.

Kwa mujibu wao, Bandari Kavu ya Kwala inaleta tumaini jipya kwa vijana (Gen Z) na wananchi kwa ujumla, kwani itafungua milango ya ajira nyingi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, hatua itakayochangia kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Wamesisitiza kuwa, ujio wa bandari hiyo umefichua fursa nyingi zilizokuwa zimejificha, huku barabara ya kuunganisha Kwala na Chalinze ikitajwa kuwa ya umuhimu mkubwa kutokana na idadi kubwa ya malori ya mizigo yanayotarajiwa kutumia njia hiyo kutoka mikoani na hata nje ya nchi.

Hatua hiyo, wamesema, itasaidia kupunguza msongamano na ajali za mara kwa mara barabara ya Morogoro.

Wananchi hao wamewasihi mawaziri wa Wizara za Uchukuzi, Ujenzi na Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI kushughulikia kwa haraka ujenzi wa barabara hiyo, wakieleza kuwa ufunguzi wa Bandari Kavu ya Kwala uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, umevutia wawekezaji wengi na kusababisha wananchi na wadau mbalimbali kuanza kununua mashamba na kuyaandaa kwa uwekezaji wa miradi ya kiuchumi.

Wamesema kukamilika kwa barabara hiyo na kuanza kwa usafirishaji wa mizigo kupitia Kwala badala ya Dar es Salaam kutafungua fursa kubwa za ajira, zikikadiriwa kufikia zaidi ya ajira milioni moja, hususan kwa vijana, na hivyo kufuta dhana potofu kuwa ajira zinapatikana mijini pekee.
Aidha, wananchi hao wamemuomba Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, kutembelea eneo la Bandari Kavu ya Kwala ili kujionea fursa zinazojitokeza na kuzisimamia kikamilifu kwa manufaa ya Watanzania.

Kwa mujibu wa wananchi hao, dhamira kuu ni kuhakikisha Watanzania wananufaika na uwepo wa bandari hiyo katika kujikomboa kiuchumi.

Miongoni mwa fursa zinazotarajiwa kujitokeza ni yadi za magari, vituo vya kuosha magari, hoteli, masoko, vituo vya mafuta na huduma nyingine za kibiashara, zitakazochangia ongezeko la kipato kwa wananchi na mapato ya Taifa kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news