DAR-Klabu ya Simba SC ya jijini Dar es Salaam imethibitisha kumteua Steve Barker kuwa kowa kocha mkuu mpya klabuni hapo akichukua mikoba ya Meneja Dimitar Pantev aliyetupiwa virago hivi karibuni.
Barker raia wa Afrika Kusini aliwahi kukutana na Simba SC kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAFCC) akiwa na Stellenbosch ya Afrika Kusini kama kocha mkuu.
Stellenbosch ilipoteza kwa bao 1-0 katika dimba la New Amaan Complex, Zanzibar kabla ya kutoshana nguvu kwa sare tasa kwenye marudiano huko Afrika Kusini.
Katika msimu huu, Barker (57) mzaliwa wa Lesotho, ameiongoza Stellenbosch kwenye michezo 24 ya mashindano yote akishinda mara nane, sare sita na kupoteza mechi 10.
Aidha,kabla ya kuiongoza Stellenbosch, Barker amewahi kuvinoa vilabu vya Mpumalanga Black Aces, Amazulu na Chuo Kikuu cha Pretoria.
