NA LWAGA MWAMBANDE
NI dhairi kuwa, katika jamii ya kisasa inayokabiliwa na changamoto nyingi za kimaadili, kijamii na kiroho,kuisema kweli ya Mungu kunabaki kuwa nguzo muhimu ya ujenzi wa maadili na ustawi wa binadamu.
Kweli ya Mungu, kama inavyofundishwa katika maandiko matakatifu, si tu mwongozo wa kiroho bali pia ni msingi wa haki, amani na mshikamano wa kijamii.
Hivyo,kuisema kweli ya Mungu kunahusisha kutangaza maadili ya haki, upendo, unyenyekevu na uwajibikaji bila woga wala upendeleo.
Aidha,katika mazingira ambayo mara nyingi ukweli hupotoshwa kwa maslahi binafsi, kisiasa au kiuchumi, sauti ya ukweli wa Mungu huwa ni sauti ya kurekebisha mwelekeo wa jamii.
Ukweli huu unawakumbusha wanadamu juu ya thamani ya utu, usawa na wajibu wao kwa wenzao.
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anabainisha kuwa, kweli ya Mungu inaweza kuangaliwa kama mfumo wa maadili unaosaidia kuunda tabia njema na maamuzi yenye tija.
Pia,tafiti nyingi za kijamii zinaonesha kuwa, jamii zinazojengwa juu ya misingi imara ya maadili huwa na viwango vya chini vya uhalifu, rushwa na migogoro.
Hivyo, kuhubiri na kuishi kweli ya Mungu kunachangia moja kwa moja katika maendeleo endelevu ya jamii na Taifa. Endelea;
1. Kweli ya Mungu hutesa, wengine wakisikia
Wasiopendezwa hasa, kweli ikiwaingia,
Kwao hiyo ndiyo fursa, ya watu kufanyiziwa,
Iseme kweli ya Mungu, hata kama utateswa.
2. Ya nabii Yeremia, watu alowaambia,
Hawakuyafurahia, kwa vile waliumia,
Nafasi wakatumia, ili aweze umia,
Iseme kweli ya Mungu, hata kama utateswa.
3. Yeremia liwambia, Bwana aliyomwambia,
Kwamba atayesalia, kifo chaweza mjia,
Bali atayekimbia, uhai utabakia,
Iseme kweli ya Mungu, hata kama utateswa.
4. Mji wanaokalia, utatekwa liwambia
Na wao kumsikia, hawakumfurahia,
Njama wakamfanyia, shimoni wakamtia,
Iseme kweli ya Mungu, hata kama utateswa.
5. Mungu aliyomwambia, ndiyo aliwaambia,
Hakuwabadilishia, waweze kumridhia,
Kweli ndiyo lisalia, ili kuwafikishia,
Iseme kweli ya Mungu, hata kama utateswa.
6. Mungu anachokwambia, watu kuwafikishia,
Usigwaye nakwambia, vitisho ukisikia,
Vema kuwafikishia, hata kama watalia,
Iseme kweli ya Mungu, hata kama utateswa.
7. Wangetaka kusikia, wanayoyafurahia,
Kwa vile wanadhania, yako unajitungia,
Kumbe unamsikia, unayemtumikia,
Iseme kweli ya Mungu, hata kama utateswa.
8. Onya kisisitizia, wasije kuangamia,
Neno ukilitumia, anavyokufunulia,
Mbali wakikutupia, usijali nakwambia,
Iseme kweli ya Mungu, hata kama utateswa.
9. Matopeni Yeremia, shimo walomtupia,
Angeweza angamia, kweli akisimamia,
Mungu akaingilia, katoka hakubakia,
Iseme kweli ya Mungu, hata kama utateswa.
10. Vivyo kimtumikia, na wakakufanyizia,
Waweza ukaishia, Stefano kumbukia,
Huku unafurahia, Yesu ukimwangalia,
Iseme kweli ya Mungu, hata kama utateswa.
11. Au akaingilia, ili kukusaidia,
Tanuruni kuingia, moto nguvu kuishia,
Simba kukuangalia, pembeni wametulia,
Iseme kweli ya Mungu, hata kama utateswa.
12. Injili ikikujia, watu weze wafikia,
Usisite kutumia, nafasi yako sikia,
Mungu takuandalia, utavyowahudumia,
Iseme kweli ya Mungu, hata kama utateswa.
13. Neno la Mungu sikia, watu huwakusudia,
Naye anakutumia, uweze wafikishia,
Vema wakimsikia, na wasipomsikia,
Iseme kweli ya Mungu, hata kama utateswa.
14. Yote yanayokujia, ujumbe kifikishia,
Kaa ukifurahia, Mungu umemsikia,
Kazi ukamfanyia, alivyohitajia,
Iseme kweli ya Mungu, hata kama utateswa.
(Yeremia 38:1-13)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602