GEITA-Katika kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, Mtandao wa Polisi Wanawake (TPF-Net) Mkoa wa Geita umeendelea kufanya matendo ya huruma kwa jamii kwa kufanya usafi wa mazingira ya kituo, kutembelea wagonjwa na kutoa msaada wa shuka 20 pamoja na vifaa mbalimbali vya usafi katika Kituo cha Afya Nyankumbu kilichopo Manispaa ya Geita.
Mwenyekiti wa mtandao huo ambaye pia ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, amewaongoza Maafisa, Wakaguzi na Askari wa TPF-Net Desemba 08, 2025, ikiwa ni sehemu ya kampeni inayolenga kuongeza uelewa na kutoa wito wa kuzuia na kutokomeza ukatili na unyanyasaji wa kidijitali dhidi ya wanawake na wasichana. Kilele cha maadhimisho haya kitafanyika Desemba 10, 2025.
Kamanda Jongo amesema kuwa, TPF-Net imeenedelea kushirikiana na wadau mbalimbali na kuunga mkono juhudi za mapambano dhidi ya ukatili unaofajwa kupitia majukwaa mbalimbali ya kidijitali, sambamba na kuhamasisha wananchi kutoa taarifa mapema wanapobaini, wanaposhuhudia au wanapokumbana na vitendo vya ukatili.
Aidha, amewataka wananchi kuepuka vitendo vya vurugu, uhalifu na uvunjifu wa amani na
kukomesha vitendo vyote vya ukatili, hususan ule unaofanywa kupitia mifumo na majukwaa ya kidijitali dhidi ya wanawake na wasichana.






