Tulieni nyumbani Desemba 9 na tukatae maandamano Tanzania

NA DIRAMAKINI

SERIKALI imewataka wananchi wasiokuwa na ulazima wa kutoka nje kesho Desemba 9,2025 kubaki majumbani kama njia ya kuimarisha usalama wakati wa maadhimisho ya miaka 64 ya Uhuru wa Tanganyika.
Wito huo umetolewa na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, alipowasilisha salamu za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Watanzania, akiwataka kuadhimisha siku hiyo kwa amani na utulivu.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, Waziri Mkuu alisisitiza kuwa wale tu wenye dharura au walio katika majukumu maalumu ya kikazi ndiyo wanapaswa kuwa katika maeneo yao ya kazi kulingana na maelekezo ya viongozi wao.

Katika hatua nyingine, Serikali imesema imejiandaa kikamilifu kukabiliana na maandamano haramu yaliyopangwa kufanyika kesho kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, alieleza kuwa Serikali haitambui maandamano hayo kwa kuwa hayajapata kibali cha kisheria.

Wazri Simbachawene amesema, maandamano hayo, ambayo yamekuwa yakihamasishwa kupitia mitandao ya kijamii, yana dalili za kuibua uvunjifu wa amani na kuchafua taswira ya taifa.

Pia,amesema kuwa,vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kudhibiti aina yoyote ya uhalifu utakaojitokeza kwa kisingizio cha maandamano.

“Maandamano haya ni haramu, hayana kibali na yako kinyume cha sheria. Kama hakuna ulazima wa kutoka, tafadhali jizuieni,”amesema waziri huyo, akitoa tahadhari kuwa yeyote atakayeshiriki atakutana na hatua za vyombo vya dola.

Akitoa rejea ya matukio ya Oktoba 29, waziri huyo alisema baadhi ya watu walijikuta wakishiriki vurugu bila kuelewa kilichokuwa kikiendelea, na kwamba maandamano yanayodaiwa kufanyika kesho yanaelezwa kuwa makubwa zaidi kuliko yale ambayo yalisababisha uharibifu wa mali, ikiwemo uchomaji wa vituo vya mafuta.

“Yale hayakuwa maandamano, ni vitendo vya mapinduzi,” alisema Simbachawene, akisisitiza umuhimu wa kulinda amani na mshikamano ambao taifa limeuenzi kwa miaka mingi.

Aidha, amezungumzia utaratibu wa ukamataji unaofanywa na baadhi ya askari, akibainisha kuwa amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillus Wambura, kuhakikisha utendaji wa askari unafuata misingi ya sheria bila kuwatia wananchi hofu.

“Askari anaenda na sare, anaripoti kwa mjumbe. Ya nini uende usiku umevaa kama ninja’?” alihoji.

Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan akizungumza na wazee wa Dar es Salaam tarehe 2 Desemba alieleza kuwa, matukio ya Oktoba 29 hayakuwa maandamano, bali jitihada za kujaribu kupindua serikali, akiyataja kuwa sehemu ya mradi mpana unaofadhiliwa kwa lengo la kuchafua taswira ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news