SINGIDA-Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani linaendelea na oparesheni maalum kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka, likilenga kuhakikisha usalama wa abiria na vyombo vya usafiri barabarani.
Kuanzia Desemba 17 hadi 19, 2025, ukaguzi umefanyika maeneo ya Mzani, Misuna na Msufini, Manispaa ya Singida, ukiongozwa na SACP Butusyo Mwambelo kwa kushirikiana na SSP Robert Sewando wa Mkoa wa Singida.
Katika operesheni hiyo, madereva, maafisa usafirishaji na abiria wamekumbushwa kufuata sheria za barabarani kama vile kuvaa mikanda, kuzingatia mwendokasi na kuhakikisha magari yako salama kwa safari.SSP Sewando alisisitiza umuhimu wa kutumia tiketi za mtandaoni na kuepuka kubeba abiria au mizigo kupita kiasi.
Kwa upande wao, baadhi ya madereva wakiongozwa na Bw. Said Sambara, walilishukuru Jeshi la Polisi kwa elimu hiyo na kuahidi kuzingatia maelekezo kwa ajili ya usalama wa wote barabarani.

