NJOMBE-Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mheshimiwa Anthony Mtaka amesema,vijana ndani na nje ya mkoa huo wana wajibu wa kulinda amani ya Tanzania, kwani wao ndiyo kizazi kinachobeba matumaini na sura ya taifa.
RC Mtaka ameyasema hayo Desemba 6,2025 katika ibada ya Jumamosi iliyofanyika Kanisa la Waadvetista Wasabato Njombe Mjini mkoani hapa.
"Amani ni tunda la haki na wajibu,ni msingi thabiti wa maendeleo yetu kama jamii na kama taifa,tunao wajibu wa kuilinda amani ya nchi yetu kwa wivu mkubwa,ni jukumu letu vijana wa leo,kuitunza amani yetu kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo waikute Mama Tanzania iliyo moja.
“Mkoa wetu bado upo salama,hauna matishio ya kihalifu,tunaendelea kujenga mazingira thabiti ya ulinzi wa watu na mali,ili kutoa fursa kwa wananchi wetu kuendelea kufanya shughuli zao za uzalishaji mali na mahangaiko yao ya kujipatia kipato cha siku.
"Usalama wa mkoa wetu, utatuongezea imani kwa wawekezaji wetu mbalimbali kuendelea kuamini kwamba Njombe ni mahala sahihi pa wao kuweka mitaji yao,wana Njombe tushikamane kuhakikisha tunaziepuka aina yoyote ya chokochoko zitakazoashiria uharibifu wa mali, uwekezaji,miradi ya umma na binafsi,au uharibifu wa uhai wa wananchi wenzetu,"amesisitiza RC Mtaka.
"Wananchi wenzangu,mkiona au kuhisi dalili yoyote hata ndogo inayoashiria uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama wa eneo lenu au maisha ya mtu,basi mtoe au utoe taarifa mapema,ulinzi shirikishi huanza na wanajamii mmoja mmoja kwa kutoa taarifa kwa wakati,"ameongeza RC Mtaka.
