Watanzania watakiwa kuendelea kudumisha umoja na mshikamano

ZANZIBAR-Watanzania wametakiwa kudumisha umoja na mshikamano ili kuepusha migawanyiko ya kidini inayochochea migogoro na mifarakano katika jamii, hatua ambayo ni muhimu katika kujenga taifa lenye amani na utulivu.
Wito huo umetolewa na Mlezi wa Jumuiya ya Fisabillah Zanzibar, Abubakar Hajji Bobea, wakati alipokuwa akizungumza na wanawake wa Kiislamu wa Zanzibar katika mkutano uliofanyika katika Msikiti wa Muembeshauri, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwaunganisha Watanzania na kuimarisha amani pamoja na maendeleo ya wananchi, bado yapo makundi yanayochochea migogoro na kuvuruga amani nchini.
Bobea amesema kuwa Watanzania bado hawajatenda haki ya kutosha kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, licha ya kazi kubwa na juhudi anazozifanya tangu alipoingia madarakani kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania.

Aidha, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mfano bora katika kuenzi na kudumisha maadili ya kujisitiri kwa wanawake, jambo linalopaswa kuigwa na wanawake wengine nchini.
Hata hivyo, amewataka wanawake hao kumuombea Rais kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kumuunga mkono ili azidi kupewa afya njema na nguvu katika utekelezaji wa majukumu yake ya kuliongoza Taifa.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Zanzibar, Ukhuti Amina Salum Khalfan, amewahimiza Watanzania kuendelea kuwa wamoja na kuacha ubaguzi unaotokana na tofauti za kidini.
Amesema amani na maendeleo ya nchi hayawezi kupatikana endapo wananchi wataendelea kugawanyika kwa misingi ya dini.

Nao wanawake walioshiriki katika mkutano huo wamesema wataendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kulinda amani ya nchi na kupinga vitendo vyote vinavyoweza kuhatarisha usalama na kusababisha migogoro nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news