Waziri Mkuu akagua ukarabati wa Soko la Majengo na kuelekeza ukamilike

NA JAMES MWANAMYOTO
OWM-TAMISEMI

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ametembelea Soko la Majengo jijini Dodoma na kukagua maendeleo ya ukarabati wa soko hilo, ambapo amemuelekeza mkandarasi Kampuni ya Azhar Construction kukamilisha ukarabati huo ifikapo mwezi Februari 2026 ili wafanyabiashara waanze kulitumia.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akitoa maelekezo kwa mkandarasi Kampuni ya Azhar Construction kukamilisha mradi, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa Soko la Majengo jijini Dodoma.

Katika kuhakikisha maelekezo yake yanatekelezwa, Dkt. Mwigulu amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko kufanya makubaliano ya kimaandishi na mkandarasi huyo kuwa, hakutakuwa na nyongeza ya muda wa ukarabati wa soko hilo ifikapo mwezi Februari, 2026.

“Serikali inataka ukarabati wa Soko ukamilike kwa wakati ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa Jiji la Dodoma, ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya kuendelea kukuza uchumi wa wafanyabiashara,” Dkt. Nchemba amesisitiza.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe (kushoto) akimkaribisha Mhe. Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, alipowasili kwa ajili ya ukaguzi wa maendeleo ya ukarabati wa Soko la Majengo jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe (kushoto) akitoa neno la utangulizi kwa Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, alipowasili kukagua maendeleo ya ukarabati wa Soko la Majengo jijini Dodoma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akielekea kukagua maendeleo ya ukarabati wa Soko la Majengo jijini Dodoma. Aliyeambatana nae ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe (kulia).

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe akimkaribisha Mhe. Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kuwa ukarabati wa soko hilo la Majengo unatekelezwa kupitia fedha za Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC).

Akieleza historia ya soko hilo la Majengo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema kuwa, soko hilo linalokarabatiwa ni la muda mrefu lilojengwa kipindi cha uhuru (1960’s) hivyo lilikuwa chakavu kiasi cha kutokidhi mahitaji ya sasa kwa muundo wake.

Mhe. Senyamule amefafanua kuwa, ukarabati wa soko hilo ulianza Mwezi Machi 2025 na ukarabati wake unategemewa kukamilika ifikapo Machi 25, 2026, hivyo ofisi yake inaendelea na juhudi za kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati licha ya maendeleo ya utekelezaji wake kutoendana na muda uliopangwa kimkataba.

Naye, mmoja wa wafanyabiashara katika Soko la Majengo, Bw. Abubakari Athuman amemshukuru Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kufanya ukaguzi wa ukarabati katika Soko la Majengo na kumuelekeza mkandarasi akamilishe ukarabati kwa wakati ili waweze kulitumia soko hilo kwani hivi sasa wanafanya biashara katika mazingira ambayo sio rafiki kibiashara.
Mmoja wa mafundi wanaokarabati Soko la Majengo jijini Dodoma, akimwaga zege kwenye moja ya nguzo iliyopo katika soko hilo linalokarabatiwa na Serikali kupitia mradi wa TACTIC.
Mfanyabiashara wa Soko la Majengo jijini Dodoma, Bw. Abubakari Athuman akimshukuru Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kumuelekeza mkandarasi kukamilisha ukarabati wa Soko la Majengo.
Mfanyabisahara wa Soko la Majengo jijini Dodoma, Bi. Khadija Abdallah akieleza furaha yake, mara baada ya Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba kumuelekeza mkandarasi kukamilisha ukarabati wa Soko la Majengo.
Mwonekano wa Soko la Majengo jijini Dodoma, ambalo linalokarabatiwa na Serikali kupitia mradi wa TACTIC.

Kwa upande wake, mfanyabisahara mwingine Bi. Khadija Abdallah amesema kufuatia maelekezo ya Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Mchemba, wafanyabiashara wamepata faraja kuwa mkandarasi atakamilisha ukarabati wa soko ili waanze kulitumia, ikizingatiwa kwamba mvua za masika zitaanza muda si mrefu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news