Waziri Mkuu aridhishwa ujenzi Bandari ya Uvuvi wilayani Kilwa

LINDI-Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba amesema ameridhishwa na kazi inayofanyika kwenye ujenzi wa bandari ya uvuvi ya Kilwa mkoani Lindi ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 90.
"Nimefurahishwa sana na maendeleo ya mradi huu ambao ni mojawapo ya miradi mingi ya kimkakati ambayo ikikamilika inaacha alama kwa Watanzania," amesema.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, Desemba 19, 2025 wakati akizungumza na viongozi na wananchi mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bandari hiyo iliyopo Kilwa Masoko, wilayani Kilwa, mkoani Lindi.
Amesema ujenzi wa bandari hiyo ya uvuvi ni mwanzo wa safari ya miradi mikubwa iliyoandikwa kwenye DIRA 2050.

"Bandari hii ni mojawapo ya miradi mingi inayofafanua kauli za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alizozitoa baada ya kuapishwa kwamba atasimamia utekelezaji wa miradi inayotoa majibu ya kero za Watanzania," amesema na kuongeza kuwa:

"Tanzania inakwenda kuandika historia mpya kwenye sekta ya uvuvi, Rais Dkt. Samia aliahidi kuendeleza miradi iliyoanzishwa na watangulizi wake na mmojawapo ni huu wa bandari ya uvuvi uliopo wilayani Kilwa."
Amesema, kukamilika kwa mradi huo, kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza kipato na kubadili maisha ya Watanzania pamoja na kuongeza pato la Taifa.

“Rais Dkt. Samia ni kiongozi ambaye anatekeleza miradi inayotoa majawabu ya kero za Watanzania. Ili kuhakikisha mradi huo unafanya vizuri, Rais Dkt. Samia ameahidi kununua meli tano za uvuvi ili kuharakisha ukuaji wa sekta ya uvuvi,” amesema.

Naye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally alisema watahakikisha kuwa bandari hiyo inazalisha ajira, inazalisha mapato na inaendelea kuwa kielelezo cha mafanikio ya Serikali.

"Kwa vile bandari hii ni ya kisasa, tumeanza mchakato wa kuithibitisha katika viwango vya kikanda na kimataifa."

Ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wadau kutoka sekta binafsi kwani wana nafasi kubwa ya kuwekeza kwenye eneo la mafuta (ya boti), viwanda vya uchakataji samaki na uendeshaji wa bandari hiyo.
Mapema, akitoa maelezo ya ujenzi wa bandari hiyo, Meneja Mradi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa, Mhandisi George Kwandu alimweleza Waziri Mkuu kwamba mradi huo utagharimu sh. bilioni 280 hadi kukamilika kwake.

"Mradi huu una eneo la ekari 48. Gati iliyojengwa ina urefu wa mita 315 na ina uwezo wa kupaki meli 10 na zikashusha mzigo kwa wakati mmoja. Jengo likikamilika, tutaweza kuhifadhi tani 1,800 za samaki kwa wakati mmoja na kuzalisha tani 100 za barafu kwa siku ambayo ni mahitaji makubwa ya wavuvi kwa sasa.”
Amesema,hadi sasa ujenzi wa mradi umefikia asilimia 90 na kwamba tayari sh. bilioni 209 zimeshalipwa. 

Amesema, pindi utakapokamilika, mradi huo utaanza kutoa ajira kwa watu 300 na katika mnyororo wa thamani, watu 30,000 watanufaika na mradi huo.

Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake mkoani Lindi kwa kukagua ujenzi wa madaraja na ukarabati wa barabara kuu ya Marendego – Nangurukuru-Lindi-Mingoyo na kisha kuzungumza na wananchi wa Somanga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here