DODOMA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) leo imesaini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano (MoUs) na taasisi tano za elimu ya juu ambazo ni Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Chuo Cha Takwimu Mashariki Mwa Afrika (EASTC), Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Makubaliano haya yanalenga kukuza matumizi ya akili unde, ubunifu katika matumizi ya data, na tafiti katika kuongeza tija kwenye uundaji wa sera na usimamizi wa sekta ya fedha.
Aidha, makubaliano hayo yana viambatisho vinavyohusisha Itifaki ya Ushirikishwaji wa Data, ambapo BoT itatoa data zilizozingatia Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, ili kuwawezesha watafiti vyuoni kupata uzoefu wa kutatua changamoto halisi, kupunguza muda wa utafiti unaosababishwa na ukosefu wa data, na kukuza ubunifu katika akili unde na matumizi ya teknolojia za kisasa za data.Gavana wa Benki Kuu amesema tukio hili ni hatua ya kimkakati katika kuimarisha ubunifu unaozingatia maadili, usalama na maslahi ya umma.















