NA DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imeeleza kuwa, kuorodheshwa kwa Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja wa iTrust Finance Limited, ujulikanao kama iTrust EAC Large Cap ETF, katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ni hatua ya kihistoria itakayochochea ukuaji wa masoko ya mitaji na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika hafla ya kuorodheshwa kwa mfuko huo iliyofanyika leo Januari 28,2026 jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, CPA Nicodemus Mkama amesema kuwa, mfuko huo ni wa kwanza nchini na katika Ukanda wa Afrika Mashariki kuwekeza katika hisa za kampuni kubwa zenye mtaji mkubwa na utendaji mzuri zilizoorodheshwa kwenye masoko ya hisa ya kikanda.
CPA Mkama amesema, kuanzishwa kwa iTrust EAC Large Cap ETF ni uthibitisho wa juhudi za Serikali kupitia CMSA katika kuendelea kubuni na kusimamia bidhaa bunifu zinazopanua wigo wa uwekezaji kwa Watanzania na wawekezaji wa kimataifa.
“Mfuko huu unaweka alama muhimu katika historia ya masoko ya mitaji nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki, kwa kutoa fursa ya uwekezaji wa kikanda kupitia soko la hisa la Tanzania,” alisema Mkama.
Vilevile ameipongeza Bodi na Menejimenti ya iTrust Finance Limited kwa juhudi zao za kubuni na kuanzisha mfuko huo, akisema kuwa hatua hiyo inaonesha ukuaji wa sekta ya fedha na kuimarika kwa imani ya wawekezaji katika masoko ya mitaji ya Tanzania.
Kwa mujibu wa CMSA, mauzo ya awali ya vipande vya mfuko huo yalivuka lengo kwa kiwango kikubwa baada ya kukusanya shilingi bilioni 54.03 sawa na mafanikio ya asilimia 540, ikilinganishwa na lengo la awali la shilingi bilioni 10.
Takwimu zinaonesha kuwa, asilimia 99.44 ya wawekezaji walikuwa ni mwekezaji mmoja mmoja huku asilimia 99.75 ikiwa ni wawekezaji wa ndani.
Mfuko wa iTrust EAC Large Cap ETF unasimamiwa na iTrust Finance Limited kama Meneja wa Mfuko, huku Benki ya NBC ikihudumu kama Mtunza Dhamana.
Aidha,mfuko huo umeidhinishwa na unasimamiwa na CMSA kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo ya masoko ya mitaji nchini.
Kwa mujibu wa sera ya uwekezaji iliyoidhinishwa, mfuko huo unawekeza katika hisa za kampuni mbalimbali kubwa zikiwemo CRDB Bank PLC, NMB Bank PLC, Vodacom Tanzania PLC, Safaricom PLC,
Pia,Equity Group Holdings PLC, KCB Group PLC, MTN Uganda Ltd, Benki ya Kigali pamoja na kampuni nyingine za kikanda zenye ukwasi na utendaji mzuri.
CPA Mkama ameeleza kuwa, mafanikio ya mfuko huo yametokana na mazingira mazuri ya kisera na kisheria, matumizi ya teknolojia kupitia mfumo wa kielektroniki wa iTrust Mobile Trading App, pamoja na elimu ya uwekezaji inayotolewa kwa umma na CMSA kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha.
Ameongeza kuwa, kuorodheshwa kwa mfuko huo kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam kunawawezesha wawekezaji kuuza na kununua vipande vyao kwa urahisi, kuongeza ukwasi sokoni na kuwawezesha wawekezaji kufahamu thamani halisi ya uwekezaji wao.
Katika hotuba yake, Afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA amewataka wasimamizi wa mfuko huo kuhakikisha wanaongeza thamani ya uwekezaji wa wanahisa kwa kuzingatia sera ya uwekezaji na kufanya maamuzi yenye tija.
Vilevile ametoa wito kwa taasisi za umma na binafsi kutumia masoko ya mitaji kama chanzo cha fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo, huku akihimiza kampuni zenye leseni kuendelea kubuni bidhaa za kifedha zitakazopanua ushiriki wa wawekezaji.
CPA Mkama amesema, CMSA itaendelea kuweka mazingira wezeshi na shirikishi kwa lengo la kuimarisha masoko ya mitaji na kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya wananchi.
Awali, uongozi wa Kampuni ya iTRUST Finance Limited umesema kuwa, mfuko wake wa uwekezaji wa iTrust EAC Large Cap ETF umefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika kipindi chake cha uuzaji wa hisa kwa umma kwa mara ya kwaza (Initial Public Offering-IPO).
Kwa mujibu wa iTrust uuzaji huo ulifanyika kuanzia Novemba 17 hadi Desemba 19,2025, ukiwa na lengo la kukusanya shilingi bilioni 10 za Tanzania.
Hata hivyo, mahitaji ya wawekezaji yalivuka matarajio baada ya watu binafsi na taasisi kuomba kuwekeza jumla ya zaidi ya shilingi bilioni 54, sawa na kiwango cha usajili cha asilimia 540.
Aidha, hadi kufikia Januari 27, 2026, thamani halisi ya mfuko (Net Asset Value-NAV) ilikuwa imeongezeka kutoka shilingi 1,000 hadi shilingi 1,064.9518, ikiwa ni ongezeko la asilimia 6.5 ndani ya kipindi cha wiki moja pekee.
Mafanikio haya yanaonesha kiwango kikubwa cha imani ya wawekezaji kwa mfuko huo pamoja na fursa za uwekezaji zilizopo katika kampuni kubwa na imara za Afrika Mashariki.
Kutokana na mwitikio huo mkubwa, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) iliidhinisha ombi la iTRUST Finance Limited la kukubali asilimia 100 ya maombi yote halali ya uwekezaji, bila kupunguza kiasi chochote kilichoombwa na wawekezaji.
Mfuko wa iTrust EAC Large Cap ETF unawekeza fedha za umma katika kampuni kubwa, zilizojengeka vizuri na zilizosajiliwa kwenye masoko ya hisa ya Afrika Mashariki. Kupitia mfuko huu, wawekezaji wanapata fursa ya kuwekeza katika kampuni nyingi kwa wakati mmoja kupitia uwekezaji mmoja.
Aidha,uongozi wa iTRUST Finance Limited umeeleza shukrani zake za dhati kwa wawekezaji wote, taasisi za serikali pamoja na wadau mbalimbali kwa ushirikiano wao uliowezesha mafanikio ya mfuko huo.
