NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imevipongeza vyombo vya habari na waandishi wa habari nchini kwa mchango wao mkubwa katika kuelimisha jamii na kuunga mkono juhudi za kitaifa za kupambana na matumizi, biashara na usambazaji wa dawa za kulevya.
Pongezi hizo zimetolewa leo Januari 9,2026 jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo wakati akifungua kikao kazi kilichoandaliwa na mamlaka kwa waandishi wa habari,kwa lengo lengo la kutathimini mchango wa vyombo vya habari katika mapambano dhidi ya changamoto ya dawa za kulevya nchini.
Pia, lengo la kikao ni kuboresha ushirikiano kati ya DCEA na vyombo vya habari, kupata namna bora katika kuripoti taarifa zinazohusu tatizo la dawa za kulevya ili kuongeza uelewa kwa jamii juu ya janga la dawa za kulevya.
Kamishna Jenerali Lyimo amefafanua kuwa, vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa umma, kufichua mitandao ya wahalifu na kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya tatizo hilo linaloathiri afya, usalama na maendeleo ya taifa.


Amesema, dawa za kulevya ni uhalifu wa kupangwa na unaovuka mipaka, hivyo vyombo vya habari vinapaswa kuendelea kushirikiana na taasisi za serikali na wadau wengine kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari,ili kuhakikisha taarifa sahihi na zenye tija zinaifikia jamii kwa wakati.
“Bila ninyi hatuwezi kufanya jambo la kuwaelimisha wananchi kuhusu dawa za kulevya, kupitia vyombo vyenu vya habari ndipo Tanzania imefahamika Dunia nzima kufanikisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya, awali Tanzania ilifanywa kuwa lango la dawa za kulevya, lakini sasa hilo lango limefungwa.
“Sisi Tanzania, hatutaki kuruhusu madhara ya dawa za kulevya katika Taifa letu, hivyo tunaendelea kushirikiana ili kuhakikisha tunaishinda vita hii kwa pamoja,"amefafanua Kamishna Jenerali Lyimo.

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA),Aretas Lyimo akifungua warsha ya siku moja ya waandishi wa habari kuhusu ushirikishwaji wa waandishi wa habari katika utoaji wa taarifa za dawa za kulevya kwa jamii.Warsha hiyo imefanyika leo Januari 9, 2026 jijini Dar es Salaam.
Amesema, kupitia vyombo vya habari wananchi wanapata uelewa wa kina kuhusu mbinu ambazo wahalifu wa dawa za kulevya wanazotumia kuingiza na kusambaza katika jamii, na pia kupata uelewa mpana kuhusu dawa mpya za kulevya.
Vilevile, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, dawa za kuleya ni moja ya silaha hatari ambayo inaweza kuua uchumi wa Taifa kwa wakati mmoja, hivyo jitihada za pamoja zinahitajika ili kuhakikisha kuwa dawa za kulevya hazina nafasi katika Taifa letu.
“Waandishi wa habari wameifanya DCEA kujulikana ndani ya nchi na nje ya nchi, kupitia makala mbalimbali na habari ambazo zimekuwa zikichapishwa katika vyombo hivyo na kuripotiwa, hivyo kuwapa uelewa watu kuhusu mapambano dhidi ya dawa za kulevya."

"Bila ninyi (waandishi na vyombo vya habari), nchi itakuwa gizani, hivyo kwa pamoja tunapaswa kuipiga vita hii kwa pamoja, kwa sababu ukiharibu vijana,umeharibu Taifa."
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)
