ARUSHA-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba ameshiriki katika shughuli za mazishi na maziko ya aliyekuwa Gavana wa Kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania, Hayati Edwin Isaac Mbiliewi Mtei, zilizofanyika jijini Arusha leo Januari 24,2024.
Akitoa salamu za rambirambi katika maziko hayo, Gavana Tutuba amesisitiza umuhimu wa kumuenzi Hayati Mzee Mtei kwa kuendeleza misingi ya kufanya kazi kwa bidii na uadilifu. 

Amebainisha kuwa, Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kumuenzi kiongozi huyo shupavu kwa kuongeza juhudi katika utekelezaji wa majukumu yake, ikiamini kuwa kazi ndiyo msingi mkuu wa maendeleo ya taifa.
Aidha, Gavana Tutuba alisema kuwa BoT, kwa dhamana iliyonayo ya kusimamia uchumi wa nchi, inaendelea kushuhudia ukuaji wa uchumi unaotokana na jitihada na utendaji kazi wa wananchi katika sekta mbalimbali.
Alisisitiza kuwa, Benki Kuu itaendelea kuweka na kusimamia sera thabiti za uchumi, mifumo ya fedha pamoja na mazingira wezeshi kwa shughuli zote za kiuchumi zinazochochea maendeleo endelevu ya Taifa.
Maziko ya Hayati Edwin Mtei yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe, Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, Gavana Mstaafu, Prof. Florens Luoga, pamoja na wananchi, wakimuenzi kwa mchango wake mkubwa katika kuanzisha na kuimarisha taasisi ya Benki Kuu ya Tanzania.




