NA LWAGA MWAMBANDE
MSHAMBULIAJI wa timu ya Taifa ya Nigeria, Victor Osimhen ambaye pia ni straika wa klabu ya Galatasaray ameibua hoja mseto ambayo licha ya kusisimua, kugusa maisha pia inatoa funzo.
Osimhen hivi karibuni amegusia uzoefu wake
kuhusu changamoto za kusaidia watu wa karibu kifedha na kukosa kuthaminiwa kwa msaada huo.
Kupitia andiko lake anaeleza kuwa, hapo awali alikuwa akimtumia fedha rafiki yake mmoja wa utotoni.
Hata hivyo, siku moja rafiki huyo alimweleza kuhusu mpango wa kuanzisha biashara na akaomba msaada wa kifedha. Osimhen alikubali na kumtumia kiasi cha Euro elfu tano (€5,000).
Kwa mshangao wake, rafiki huyo hakuthamini msaada huo na badala yake alimwambia kuwa alisoma kwenye vyombo vya habari kuwa, yeye Osimhen alikuwa akipata zaidi ya Euro milioni moja kwa wiki, hivyo alitarajia kupokea Euro elfu hamsini (€50,000) kwa ajili ya kuanzisha biashara hiyo.
Osimhen anasema hali hiyo ilimkasirisha sana hadi akatamani kusitisha muamala huo, lakini hakuweza.
Nyota huyo wa soka barani Afrika anaeleza kuwa, ingawa Euro elfu tano zinaweza kuonekana kuwa ni kiasi kidogo barani Ulaya, nchini Nigeria ni fedha nyingi zenye uwezo wa kubadilisha maisha ya mtu.
Ameongeza kuwa,kabla ya kwenda Ulaya, hakuwahi kupata msaada wa kifedha kutoka kwa mtu yeyote, bali alijituma kwa bidii, akifanya kazi ndogondogo ikiwemo kuuza maji barabarani ili kujikimu.
Osimhen anasisitiza kuwa, jamii inapaswa kujifunza kuthamini chochote wanachopewa kama msaada na kuacha kuwa na mtazamo wa kudai au kujiona wanastahili zaidi, akieleza kuwa mafanikio yanahitaji juhudi, subira na shukrani.
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasema kuwa,ujumbe wa Victor Osimhen umebeba funzo muhimu kuhusu maadili, shukrani na uhalisia wa maisha nyuma ya mafanikio ya watu, hivyo tuwe na shukrani.Endelea;
1. Kuweni na shukurani, chochote mnachopewa,
Acha roho ya kwanini, wakati mwasaidiwa,
Ni Victor Osimheni, somo sote twapatiwa,
Kitu kile wewe huna, pokea sema asante.
2. Ni mchezaji mahiri, wa soka twamuelewa,
Hii ya kwake habari, ni sisi tunaambiwa,
Haya sawa mahubiri, kama vema twaelewa,
Kitu kile wewe huna, pokea sema asante.
3. Mchezaji wa Mpira, hadithi tunaambiwa,
Aliona yeye bora, nyumbani kusaidiwa,
Ni sadaka si hasara, rafiki walipatiwa,
Kitu kile wewe huna, pokea sema asante.
4. Mara rafiki mmoja, kaomba kusaidiwa,
Mtaji ni yake haja, biashara kutumiwa,
Ikawa ni nzuri hoja, mtaji ule kapewa,
Kitu kile wewe huna, pokea sema asante.
5. Ni Euro elfu tano, ambazo alipatiwa,
Shilingi kumi na tano, milioni lizopewa,
Kitita kizuri mno, na mtu kusaidiwa,
Kitu kile wewe huna, pokea sema asante.
6. Badala ya kushukuru, kiasi alichopewa,
Uso ukakosa nuru, vile hakutegemewa,
Ampe zile ndururu, ndogo sana kaambiwa,
Kitu kile wewe huna, pokea sema asante.
7. Pesa zile alitaka, naye Victor kupewa,
Hamsini alitaka, elfu Euro angepewa,
Efu tano takataka, ndivyo alivyoelewa,
Kitu kile wewe huna, pokea sema asante.
8. Somo tunalofundishwa, tupasalo kuelewa,
Ni zuri si la kuchoshwa, pale tunasaidiwa,
Ni vema tukaridhishwa, na kile tunachopewa,
Kitu kile wewe huna, pokea sema asante.
9. Pesa hii haitoshi, kotekote yawaniwa,
Watu haiwaridhishi, yatafutwa sawasawa,
Mtu akikupa keshi, jua umependelewa,
Kitu kile wewe huna, pokea sema asante.
10. Pesa yasakwa kwa jasho, ili ipate tumiwa,
Kama hujatoa jasho, halafu pesa wapewa,
Acha kuwa wa michosho, kwa dharau kupokewa,
Kitu kile wewe huna, pokea sema asante.
11. Uwe nayo shukuruni, kama kitu umepewa,
Hiyo ujue ni dini, ndivyo tunavyoambiwa,
Vinginevyo ni uhuni, kesho tena hutapewa,
Kitu kile wewe huna, pokea sema asante.
(1 Wathesalonike 5:18)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
