DODOMA-Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imefanya zoezi la upandaji miti katika Skimu ya Umwagiliaji Hombolo, mkoani Dodoma, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za kitaifa za uhifadhi wa mazingira na utunzuaji wa rasilimali za maji.
Hafla hiyo imefanyika kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa mkoa, akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amesisitiza umuhimu wa kulinda mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Amesema kuwa,Rais Samia Suluhu Hassan ameamua kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa kupanda miti, jambo alilolieleza kuwa ni utashi wa kipekee wa kuonesha uzalendo katika utunzaji mazingira.
Hafla hiyo ya kupanda miti imefanyika ikiwa na kauli mbiu inayosema: “Uzalendo ni kutunza Mazingira, shiriki kupanda miti.”
Senyamule amesema kuwa Dodoma imeamua kuunga mkono jitihada za Rais kwa kuanzisha Kauli mbiu isemayo: “siku yangu ya kuzaliwa, mti wangu. Hii ni dhana ya kuacha alama ya kudumu kwa kuhakikisha kuwa kila mwananchi anaazimisha siku yake ya kuzaliwa kwa kupanda miti,” amesema huku akiwasihi wananchi wa Dodoma kuiga mfano huo kwa kupanda miti katika makazi yao.
“Hombolo endeleeni kutunza hili bwawa, kwani bwawa hili ndiyo chakula na ndiyo uchumi,” alihimiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIRC Raymond Mndolwa, alisisitiza kuwa zoezi la upandaji miti nchi nzima ni endelevu na litahusisha wakulima ili kulinda vyanzo vya maji vinavyoayhiria na shughuli za binadamu.
Ameongeza kuwa watoto watakaotunza miti watatuzwa, ili kuhamasisha kizazi kipya kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira.
Sambamba na upandaji miti, NIRC imepanga kufanya ukarabati wa bwawa la Hombolo ili kulinda chanzo cha maji na kuhakikisha wakulima wanaendelea kunufaika na kilimo cha umwagiliaji.
Mndolwa ameongeza kuwa, zoezi hili ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Mifumo himilivu ya Chakula nchini (TFSRP-P4R), ili kuhakikisha miradi ya Umwagiliaji inajengwa kwa misingi ya ustahimilivu wa tabianchi, ikilinda vyanzo vya maji na kuimarisha maisha ya wakulima.
“Tunapanda miti, tunatunza bwawa, na tunajenga uchumi wa jamii,” amesisitiza.
Hafla ya upandaji miti ni alama ya matumaini katika kulinda mazingira na vyanzo Maji.
Tags
Habari
Kilimo cha Umwagiliaji
NIRC Tanzania
Skimu ya Hombolo
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC)
Watumishi NIRC















