NA DIRAMAKINI
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Baraka Hassani Juma (19), mkazi wa Kagongwa, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, kwa tuhuma za kumtorosha mwanafunzi wa kike mwenye umri wa miaka 14, anayesoma kidato cha pili, ambaye jina lake limehifadhiwa kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, tukio hilo linadaiwa kutokea Januari 5, 2026 katika Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, kufuatia ufuatiliaji wa kina uliofanywa na Jeshi la Polisi, mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 17, 2026 katika nyumba ya kulala wageni iliyopo eneo la Ukonga Mombasa, Dar es Salaam, akiwa pamoja na mwanafunzi huyo, wakijiandaa kuondoka na kuelekea Kagongwa, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa, uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na kwamba hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa kwa kushirikiana na mamlaka nyingine husika

