Rais Dkt.Samia atoa ndege maalum kwenda kuwachukua wachezaji wa Taifa Stars

DAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa ndege maalum (Boeing 787-8 Dreamliner) kwa ajili ya kwenda nchini Morocco kuwachukua wachezaji wa timu ya kandanda ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ambao walikuwa wanashiriki mashindano ya AFCON na kuwarejesha jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, amesema Mhe. Rais Samia, ametoa ndege ya kuwasafirisha wachezaji, benchi la ufundi na viongozi walioko Morocco wakiongozwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda ikiwa ni kutambua heshima kubwa waliyolijengea Taifa la Tanzania katika mashindano hayo makubwa Barani Afrika licha ya kuondolewa na wenyeji Morocco katika hatua ya 16 ambayo hawakuwahi kuifikia.

Pamoja na kuwatumia ndege ya kuwasafirisha Taifa Stars kutoka Morocco kurejea Tanzania, Mhe. Rais Samia, ameandaa hafla ya chakula cha mchana itakayofanyika tarehe 10 Januari, 2026, katika Ikulu ya Magogoni, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuwapongeza rasmi Taifa Stars pamoja na wanamichezo wengine waliofanya vizuri katika michezo mbalimbali.

Ndege maalum iliyotolewa na Mhe. Rais Samia, aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, inatarajiwa kuondoka jijini Dar es Salaam, kesho tarehe 6 Januari, 2026; majira ya saa 9:00 alasiri na itawasili jijini Rabat, Morocco, kesho hiyo hiyo majira ya saa 4:30 usiku, kisha itaondoka jijini Rabat, Morocco tarehe 7 Januari, 2026, na kuwasili jijini Dar es Salaam, siku hiyo majira ya saa 2:00 usiku, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here