NA LWAGA MWAMBANDE
KILA mwanadamu amepewa karama au kipaji maalum kutoka kwa Mungu kwa kusudi maalum, ingawa karama hiyo haiwezi kuleta manufaa iwapo haitachochewa na kuendelezwa.
Kuchochea karama kunahusisha kuitambua, kuiombea kwa Mungu, kuikuza kupitia elimu na mazoezi, na kuitumia kwa nidhamu na uwajibikaji.
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande, anabainisha kuwa,karama inahitaji bidii, kujifunza na maadili mema ili ikue na kuzaa matunda.
Aidha,inapotumiwa kwa unyenyekevu na kwa manufaa ya jamii, huleta maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla. Hivyo,ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha karama aliyopewa haipotei, bali inachangia ujenzi wa jamii yenye tija na maadili.
1. Linasema yafueni, majembe yawe mapanga,
Miundu yenu nyumbani, mikuki ya kuwalenga,
Mdhaifu wa mwilini, aseme amejipanga,
Neno la Mungu lasema, chochea karama yako.
2. Kwenye eneo lolote, hakiki unajipanga,
Mema uyafanye yote, kama njaa unaganga,
Na wala usitepete, kutumika ukavunga,
Neno la Mungu lasema, chochea karama yako.
3. Mungu amekuandaa, jinsi alivyokujenga,
Uache kukaakaa, si mwanamwali mjinga,
Unachofanya komaa, kesho yako waijenga,
Neno la Mungu lasema, chochea karama yako.
4. Pengine wewe mwalimu, vema sana kujipanga,
Udumu ukihudumu, wengine ukiwajenga,
Wakishapata elimu, tofali umeshapanga,
Neno la Mungu lasema, chochea karama yako.
5. Usifanye kidhaifu, kama mjingamjinga,
Wala usiwe na hofu, karama wajaza tenga,
Kazi ndio unadhifu, fanya bila chengachenga,
Neno la Mungu lasema, chochea karama yako.
6. Uwe umejiandaa, hila zote kuzipinga,
Zile zitazokuvaa, naye Mungu kukutenga,
Ulipo wewe kata, imani zidi kujenga,
Neno la Mungu lasema, chochea karama yako.
7. Waseme hujajipanga, useme umejipanga,
Waone mwamba wagonga, wewe mbele zidi songa,
Tumika bila kuvunga, milele unaijenga,
Neno la Mungu lasema, chochea karama yako.
8. Hakiki wakati wote, kwamba wewe ni upanga,
Unafyeka vile vyote, vinavyoleta ujinga,
Ufanyayo mambo yote, vizuri unayachonga,
Neno la Mungu lasema, chochea karama yako.
9. Kama mkuki mkuki, choma bila kujivunga,
Na tena hapo hakiki, vizuri umejijenga,
Akija mwovu hatoki, aende na wake wanga,
Neno la Mungu lasema, chochea karama yako.
10. Yeye akija kimwili, kiroho umejipanga,
Kwa maombi mkabili, mishale ikimlenga,
Azime kama kandili, apate la macho changa,
Neno la Mungu lasema, chochea karama yako.
(Yoeli 3 :10)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602